Ligi kuu ya soka Tanzania bara itaendelea tena mwishoni mwa
juma hili kwa michezo kadhaa kuunguruma kwenye viwanja tofauti, ambapo
katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam Wekundu wa MSimbazi Simba
watakuwa na kibarua cha kuwakabili Stand Utd (CHAMA LA WANA) kutoka
mkoani Shinyanga.
Simba wataingia uwanjani hiyo kesho huku wakiwa na kumbu kumbu ya
matokeo ya sare mbili mfululizo dhidi ya Polisi Morogoro pamoja na
Costal Union hivyo watahitaji kurejesha matumaini kwa mashabiki wao kwa
kuhakikisha ushindi wao wa kwanza msimu huu katika ligi ya Tanzania bara
unapatikana.
Kwa upande wa Stand Utd, wameingia jijini Dar es salaam wakiwa na
chagizo la ushindi wa bao moja kwa sifuri walioupata jijini Tanga katika
uwanja wa CCM Mkwawani mbele ya wenyeji wao Mgambo JKT, hivyo watafanya
njia zote za kutaka kuendeleza shangwe la ushindi mbele ya mnyama.
Mkoano Morogoro maafande wa jeshi la polisi mkoani humo kesho
watacheza mchezo wao wa kwanza msimu huu katika uwanja wa nyumbani wa
Jamuhuri dhidi ya wakata miwa kutoka mkoani Kagera, Wanankurukumbi
Kagera Sukari.
Katika uwanja wa CCM Mkwawakni jijini Tanga wenyeji wa jiji hilo
Costal Union nao watakuwa mbele ya mashabiki wao kwa mara ya kwanza
tangu msimu huu ulipoanza kwa kuhakikisha wanasaka ushindi mbele ya
Ndanda Fc kutoka mkoani Mtwara.
Huko jijini Mbeya maafande wa Tanzania Prisons nao watakuwa
wanajaribu kuwaweka korokoroni mabingwa wa soka Tanzania bara Azam FC
katika uwanja wa Sokoine.
Ikumbukwe kwamba Azam FC imeshinda michezo yao miwiwli iliyopita
dhidi ya Ruvu Shooting pamoja na Polisi Morogoro hivyo nao hawatokuwa
tayari kuharibiwa mpango wa kutaka kuendeleza wimbi la ushindi hiyo
kesho.
Kwa upande wa Tanzania Prisons watahitaji kushinda mchezo huo kwa
minajili ya kufuta makosa waliyoyafanya katika mchezo wao uliopita
ambapo walikubali kufungwa na Dar es salaam Young African katika uwanja
wa taifa mwishoni mwa juma lililopita mabao mawili kwa moja.
Mkoani Pwani katika uwanja wa Mabatini uliopo maeneo ya Mlandizi
kesho kutakuwa na mtanange kati ya Mbeya City dhidi ya Ruvu Shooting.
Siku ya jumapili kutakuwa na michezo miwiwli ya ligi kuu ya soka
Tanzania bara ambapo katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam
kutakuwa na mpambano kati ya Dar es salaam Young Africans dhidi ya JKT
Ruvu na mkoani Morogoro katika uwanja wa Manungu uliopo maeneo ya
Turiani Mtibwa Sukari watawakaribisha Mgambo JKT kutoka wilayani Handeni
mkoani Tanga.
0 comments:
Chapisha Maoni