Alhamisi, Septemba 18, 2014

WAFANYA BIASHARA MBEYA WATAKIWA KUSAJILI BIASHARA ZAO

WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya, wametakiwa kusajili majina ya biashara zao kama moja ya njia ya kuzirasimisha na hatimaye kuwa na uwezo wa kufaidika na huduma za kibenki.
Rai hiyo ilitolewa mjini Mbeya na Meneja Uhusiano wa Benki ya NMB, Nyanda za Juu Kusini, Focus Lubende, alipokuwa akishiriki kutoa mafunzo kwa wajasiriamali na wafanyabiashara waliohudhuria semina ya mafunzo inayoendeshwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
Sajilini majina ya biashara zenu, ili tuwatambue na muweze kufaidika na mikopo kuendeleza biashara zenu
alisema.
Brela inaendesha mafunzo kwa wakazi wa mkoa wa Mbeya kuhusiana na kazi wanazofanya na jinsi wafanyabiashara wanavyoweza kufaidika na huduma zao.
Ofisa Uhusiano huyo aliwataka wafanyabiashara hao kujenga mazoea ya kuweka akiba benki, ili kuzidi kupanua biashara zao.
Mfanyabiashara, Mohamed Honde aneyejishughulisha na utengenezaji vyerehani, aliishukuru Brela kwa uamuzi wa kutoa elimu kwao.
Honde alitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake ambao hawajajisajili kujisajili, kwani kwa kufanya hivyo kunatoa fursa za kupata mikopo itakayowaendeleza katika biashara zao.
Msajili Msaidizi Mwandamizi wa Brela, Rehema Kitambi lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa wafanyabiashara au wajasiriamali wadogo na wakati wa mkoa wa Mbeya kuhusu umuhimu wa kusajili biashara zao na kusajili majina ya biashara zao.

0 comments:

Chapisha Maoni