Alhamisi, Septemba 18, 2014

POLISI WAWAPIGA NA KUWANYANYASA WAANDISHI WA HABARI DAR ES SALAAM

MUENDELEZO wa Jeshi la Polisi nchini kuwanyanyasa, kuwatisha waandishi wa habari na kuwafanya wasitekeleze wajibu wao ipasavyo, ilijidhihirisha wazi jana makao makuu ya jeshi hilo, baada ya waandishi kupigwa, kukimbizwa na mbwa ili wasichukue taarifa za kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Tukio la kupigwa na kudhalilishwa kwa waandishi wa habari lilitokea jana, limetokea ikiwa ni siku moja baada ya Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini kushirikiana na waandishi wa habari katika kufanya kazi kwa ajili ya kulinda amani ya nchi.
Waandishi waliyopigwa na Polisi hiyo jana ni Josephat Isango anayeandikia gazeti hili, huku Yusuph Badi ambaye ni mpiga picha wa magazeti ya serikali, akipigwa na ‘kusakiziwa’ mbwa ili wamuume.
Dalili za waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi yao, zilianza kujionesha mapema jana wakati Mbowe alipowasili katika makao makuu ya Jeshi la Polisi, ambako waandishi walizuiwa wasiingie katika eneo hilo kwa ajili ya kuchukua picha na maelezo ya kiongozi huyo.
Akiwa anawaongoza askari wake katika amri ya kushambuliwa kwa waandishi wa habari hiyo jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisikika mara kwa mara akiwaagiza vijana wake wawaondoe waandishi na hata kuwasakizia mbwa.
Chagonja, alisikika mara kadhaa akitoa amri kwa askari kuwa wawafungulie mbwa ili waweze kujeruhi angalau mtu mmoja kutoa funzo ili wafuasi wa CHADEMA waliokuwa kwenye lango kumsubiri Mbowe waondoke.

0 comments:

Chapisha Maoni