Ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waumini na viongozi
mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya ya Ziwa
Tanganyika ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa
wakfu kwa Askofu Ambele Anyigulile Mwaipopo aliyeteuliwa kuongoza
dayosisi hiyo.
Waziri Mkuu alikuwa akitoa ufafanuzi wa hoja ya Askofu Mwaipopo
aliyetaka maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yaheshimiwe, na Bunge
Maalum la Katiba lisitishwe kama ambavyo Jukwaa la Katiba limetaka na
pia tamko la Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT)
Waziri Mkuu amesema Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume hiyo
siyo Katiba bali ni mawazo yaliyokusanywa ambayo yanapaswa kupitiwa na
chombo kingine cha kisheria ambacho ni Bunge Maalum la Katiba.
Amesema muda ambao Tume hiyo ilipewa haukuwa mrefu sana kwa hiyo
isingekuwa rahisi kwa wajumbe wake kuzingatia kila eneo linalogusa
maisha ya Watanzania.
Mh. Pinda amesema kinachowachanganya Watanzania ni suala la Serikali
mbili au tatu lakini katika makabrasha ya Tume ambayo wajumbe wote
walipewa, suala la Muungano halikupewa kipaumbele na Watanzania wengi
waliotoa maoni yao.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Tume ya mabadiliko ya katiba
watu waliotaka Muungano wa Serikali tatu ni kati ya asilimia 12 na 13
hivyo Haiwezekani takwimu hizo zitajwe kama matakwa ya Watanzania
wengi.”
Waziri Mkuu amesema yuko radhi ifanyike kura mahsusi ya kuwaomba
Watanzania waseme kama wanataka Muungano na tena uwe ni wa aina gani.
Aidha Amewasihi Maaskofu, wachungaji na viongozi wengine wa dini
waliohudhuria uzinduzi huo waendelee kuuombea mchakato huo wa katiba
ili uishe vizuri.
Katika hatua nyingine bunge maalum la katiba limeahirisha shughuli ya
uwasilishaji wa rasimu uliokuwa ufanyike leo bungeni mjini Dodoma, ili
kutoa muda kwa kamati ya uandishi kukamilisha shughuli hiyo na
kuwasilisha keshokutwa Jumatano.
0 comments:
Chapisha Maoni