Jumatano, Agosti 06, 2014

WAALIMU WA HISABATI NA SAYANSI NI KITENDAWILI CHUNYA

Zaidi ya wanafunzi 300 wanaosoma katika shule ya sekondari Saza wilayani Chunya hawana mwalimu hata mmoja wa masomo ya sayansi wala hisabati, hali ambayo inasababisha washindwe kupata elimu bora na kutishia kushindwa kufaulu mitihani yao. 
Licha ya mradi wa ujenzi wa maabara ya kisasa wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 kutekelezwa katika shule ya sekondari ya Saza, shule hii imebainika kutokuwa na mwalimu hata mmoja wa masomo ya sayansi wala hisabati hali ambayo inatishia mustakabali wa elimu kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Saza, mwalimu Peter Eliya amethibitisha shule yake kutokuwa na mwalimu hata mmoja wa masomo ya sayansi wala hisabati, huku kaimu afisa elimu wilaya ya Chunya, Lawlence Kabuje akisema kuwa tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi linaikabili wilaya nzima ya Chunya, tatizo ambalo amedai kuwa linatokana na mgawo mdogo wa walimu hao wanaoupata kutoka wizarani. 
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ameagiza suala hilo kushughulikiwa haraka ili wanafunzi hao wapate elimu wanayostahili, huku akiwaasa wananchi wa wilaya ya Chunya kuwekeza zaidi kwenye elimu ya watoto wao.

0 comments:

Chapisha Maoni