Alhamisi, Agosti 28, 2014

POLISI AMGONGA MTOTO NA GARI KISHA KUKIMBIA

Polisi mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja, aliyekuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi, Jumapili iliyopita alimgonga mtoto wa kike, Zahara Almeda katika barabara ya Mji Mpya.
Katika tukio ambalo mwandishi wa habari hizi alilishuhudia, mara tu baada ya kumgonga mtoto aliyekuwa akitoka sokoni kununua magimbi na mihogo, askari huyo aliteremka na kukimbia akiliacha nyuma gari lake lililokuwa bado halijazimwa, ambalo ndani yake kulikuwa na kofia yake.
Wananchi waliojawa na hasira baada ya tukio hilo walilizingira gari hilo na kutaka kulichoma moto, lakini busara za baadhi yao ziliwezesha kitendo hicho kutofanyika na baadaye trafiki alifika kudili na tatizo hilo
Mmoja wa watu walioshuhudia ajali hiyo iliyolihusu gari aina ya Toyota Baloon lenye namba za usajili T 553 AUE, alisema mtoto aliyegongwa alikuwa akitokea sokoni Mji Mpya, akiwa amebeba kikapu kichwani.
Mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Sudi Kiwamba, alisema binti huyo alikuwa ameshavuka barabara, lakini wakati akijiandaa kuvuka msingi wa pembeni gari hilo lilimfuata katika jitihada za kumkwepa mwendesha pikipiki.
Hata hivyo, siku moja baada ya tukio hilo, mwandishi wetu alizungumza na baba mzazi wa mtoto huyo alisema mwanaye anaendelea vizuri na mtu aliyemgonga alikwenda hospitalini kumjulia hali kwani aliamini alikuwa amefariki.

0 comments:

Chapisha Maoni