Tarehe 5 Agosti miaka 54 iliyopita nchi ya Burkina Faso ilipata
uhuru. Nchi hiyo ilikoloniwa na Ufaransa kuanzia katikati mwa karne 19.
Burkina Faso ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Upper Volta, ilijitangazia
mamlaka ya kujiendeshea mambo yake ya ndani mwaka 1958 baada ya
kutangazwa mfumo wa jamhuri lakini ilibakia mwanachama wa jamii ya
Ufaransa. Miaka miwili baadaye katika siku kama hii ya leo Burkina Faso
ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Mwaka 1984
jina la Upper Volta lilibadilishwa rasmi na kuwa Burkina Faso.
Na siku kama ya leo miaka 24 iliyopita Mawaziri wa Mambo ya Nje wa
nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu walipasisha
Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu katika mkutano uliofanyika Cairo,
nchini Misri. Kwa mnasaba huo siku hiyo imepewa jina la 'Siku ya Haki
za Binadamu za Kiislamu na Utukufu wa Mwanadamu.' Tangazo hilo lina
utangulizi na vipengee 25. Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu
lilipasishwa baada ya nchi za Kiislamu kukosoa Tangazo la Haki za
Binadamu lililopasishwa mwaka 1948 katika Umoja wa Mataifa ambalo
lilibuniwa kwa misingi ya fikra za kiliberali za nchi za Magharibi na
baadhi ya vipengee vyake vinapingana na mafundisho ya Kiislamu. Sifa kuu
inayotofautisha Azimio la Haki za Binadamu za Kiislamu na lile la Umoja
wa Mataifa ni kutilia maanani haki za kiroho na kimaanawi za maisha ya
mwanadamu kwa mujibu wa mafundisho ya Mwenyezi Mungu.
0 comments:
Chapisha Maoni