MKAZI wa Kijiji cha Mwamkuru, Wilaya ya Mpanda, Suzana Kingi
(40), ameuawa kwa kukatwa katwa na mapanga shingoni, kichwani na
mikononi na mtu asiyejulikana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema
jana kuwa mauaji hayo yalitokea juzi, saa 9 usiku nyumbani kwa Suzana
kijijini hapo alipokuwa akiishi.
Alisema siku ya tukio Suzana alikuwa amelala nyumbani kwake peke
yake jirani na nyumba waliokuwa wakiishi wakwe zake, Maria Kayungiro
na Maria Nsabi pamoja na mtoto wake aitwaye Paul Charles.
Alisema wakati Maria Kayungiro akiwa chumbani kwake alimsikia
Suzana akikimbia kutoka kwenye nyumba yake kuelekea kwenye nyumba ya
mtoto wake, Paulo huku akipiga mayowe ya kuomba msaada.
Kamanda Kidavashari alieleza wakati huo muuaji huyo alikuwa
akimfuata. Alipofika katika nyumba hiyo, mtoto wake hakuwepo, kwani
alikuwa amekwenda kwenye harusi kijiji cha jirani na ndani ya nyumba
alikuwemo Maria Nsabi.
Muuaji aliingia ndani na kuanza kumkatakata Suzana huku akimmulika kwa tochi Maria Nsabi pamoja na kumtishia kuwa akipiga kelele naye atamuua
alisema.
Kamanda Kidavashari alisema uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo
cha mauaji hayo ni imani za kishirikina na hakuna mtu aliyekamatwa
kuhusiana na tukio hilo.
0 comments:
Chapisha Maoni