Alhamisi, Julai 03, 2014

MAKAMU WA RAIS BILAL AKUTANA NA RAIS WA BURUNDI

Makamu wa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Mohammed Gharib Bilal, Amekutana na Rais wa Burundi Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza na kufanya naye mazungumzo. Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi ya Rais Nkurunzinza iliyopo katikati ya jiji la Bujumbura.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walipata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano baina ya Tanzania na Burundi ambapo Mheshimiwa makamu wa rais alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Nkurunzinza na watu wa Burundi kwa sherehe zilizofana za kutimiza miaka 52 ya uhuru. Pia alitumia nafasi hiyo kumtakia kila la heri mheshimiwa Rais Nkurunzinza pamoja na watu wa Burundi kufuatia kupiga hatua kubwa za kimaendeleo sambamba na kuweza kuwafanya wananchi wa Burundi kuwa wamoja.
Pia alimueleza Rais Nkurunzinza kuhusu umuhimu wa kuzidi kuifanya Burundi kuwa nchi moja kwa kuwaunganisha watu wake na akaeleza kuwa,Tanzania inafurahi kuona hatua kubwa za kimaendeleo zikipigwa nchini Burundi na kwamba ili hatua hizo ziwe madhubuti, upo umuhimu wa kuwafanya wananchi wa burundi kubakia wamoja na wanaoshirikiana katika kuiendeleza nchi yao.
Burundi ikifanya vizuri maana yake ni kuwa afrika mashariki imefanya vizuri. Tanzania tutafurahi na nchi zote za ukanda wetu zitafurahi
alisema mheshimiwa makamu wa Rais na kuongeza kuwa lengo la Tanzania siku zote ni kuona jirani zake wakiishi kwa utulivu na wakifanya mambo yao ya maendeleo katika hali ya amani.
Katika mazungumzo hayo rais Nkurunzinza aliendelea kuishukuru Tanzania kwa uhusiano wake wa karibu na Burundi na akaongeza kuwa wananchi wa nchi yake wamefurahishwa sana kwa Tanzania kushiriki katika sherehe za miaka 52 ya uhuru wa Burundi,sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Prince Louis Rwagasore jana. Pamoja na mheshimiwa makamu wa Rais wa Tanzania, sherehe hizo pia zilihudhuriwa na makamu wa Rais wa Somalia na waziri mkuu wa Chad.

0 comments:

Chapisha Maoni