Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukumbu ya Siku
ya Mashujaa itakayofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja
jijini Dar es salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa
Mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki amesema kuwa maadalizi ya
sherehe hizo yamekamilika na kuongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu
kihistoria yanalenga kuwaenzi wote waliojitoa muhanga katika jitihada
za kuikomboa ardhi ya Tanzania, kuilinda na kudumisha amani na utulivu
uliopo.
Amesema maadhimisho hayo yatapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo
Gwaride la Kumbukumbu litakaloonyeshwa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama
vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Jeshi la Magereza na
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Ameongeza kuwa katika maadhimisho hayo kutakuwa na uwekaji na silaha
za asili, maua kwenye mnara wa kumbukumbu pamoja na viongozi wa
madhehebu mbalimbali ya dini kutoa dua na sala kuliombea taifa.
Bw. Sadiki amefafanua kuwa shughuli zote katika viwanja vya Mnazi
Mmoja zitaanza saa mbili Asubuhi na kumalizika saa sita mchana, pia
wananchi watakaohudhuria kumbukumbu hiyo watapata fursa ya kushuhudia
matukio yatakayokuwa yananendelea uwanjani hapo kupitia Luninga kubwa
zitakazokuwepo katika maeneo yote muhimu ya uwanja huo.
Aidha, katika hatua nyingine ameeleza kuwa wakati wa maadhimisho
hayo barabara ya Lumumba, Uhuru na Bibi Titi zitafungwa kwa muda kwa
lengo la kuhakikisha usalama kwa watumiaji wa barabara hizo
watakaohudhuria maadhimisho hayo.
0 comments:
Chapisha Maoni