Jumapili, Juni 08, 2014

WAZIRI AIBIWA GESTI

WIMBI la uhalifu limeendelea kushamiri katika nyumba za wageni hapa nchini ambapo safari hii watu wanaodhaniwa kuwa ni vibaka wamemwibia nguo na fedha Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi, Dk. Titus Kamani.
Waziri huyo amekutwa na tukio hilo usiku wa kuamkia jana akiwa amelala kwenye hoteli ya Stop Over iliyopo Bariadi mjini mkoani Simiyu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alithibitisha kutokea kwa wizi huo uliofanywa na watu wanaodhaniwa ni vibaka katika hoteli aliyokuwa amelala Waziri Kamani.
Mkumbo, alisema vibaka hao walitoboa dirisha la chumba alichokuwa amelala Waziri Kamani bila mwenyewe kujua na kuzivuta nguo zake alizokuwa amezitundika ukutani.
Alisema vibaka hao walifanikiwa kuondoka na suruali ya Waziri Kamani, iliyokuwa na sh 100,000 ndani.
Ndugu mwandishi wa habari ni kweli limetokea tukio la Waziri Kamani kuibiwa akiwa amelala hotelini hapa Bariadi, kwani unataka kuandika habari hizi? Usiandike maana jamii itachukulia tukio hili tofauti.
Wezi hawa walikuwa ni vibaka tu, kuna kitambulisho cha waziri na baadhi ya nyaraka vilikuwa vimetupwa chini na mimi nimefika hotelini hapo kujionea
alisema RPC Mkumbo.
Akifafanua zaidi, alisema siku hiyo umeme ulikuwa umekatika na tayari mlinzi wa hoteli hiyo amekamatwa na kuhojiwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Mlinzi wa hoteli hiyo tumemkamata na kumhoji maana amefanya uzembe katika lindo lake la kazi na kusababisha wizi huo na tunafanya upelelezi kubaini watu waliomwibia Waziri Kamani
alisema RPC Mkumbo.
Hata hivyo Tanzania Daima Jumapili, lilipomtafuta Waziri Kamani kwa simu ili kuzungumzia tukio la kuibiwa, hakupatikana kwani simu zake zilikuwa zimezimwa.
Tukio kama hilo liliwahi kumkumba aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima huko mkoani Morogoro katika hoteli aliyokuwa amelala.

0 comments:

Chapisha Maoni