Washtakiwa watatu wakiwemo walezi na baba mzazi wa mtoto Nasra
Rashidi, waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama na kumfanyia
ukatili mtoto huyo, wamerudishwa upya polisi kwa ajili ya kuhojiwa,
baada ya mtoto huyo kufariki dunia Juni mosi mwaka huu, katika hospitali
ya taifa ya muhimbili.
Katika kesi hiyo iliyovuta umati mkubwa wa watu,
waliojaribu kuwapiga washtakiwa hao kabla ya jaribio lao kuzimwa na
polisi, hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa
Morogoro, Mary Moyo, ameridhia washtakiwa hao, Mariam Said, Mtonga Omary
na Rashid Mvungi, warudishwe upya kituo kikuu cha polisi Morogoro kwa
mahojiano ya awali, kama walivyoshauri waendesha mashtaka watatu wa
serikali, Sunday Hyera, wakili wa serikali Edgar Bantulaki na inspekta
wa polisi Zablon Msusi, na kesi hiyo ifikishwe tena mahakamani hapo Juni
12 kwa ajili ya kutajwa, na kwamba baada ya mahojiano washtakiwa hao
warudishwe mahali husika kwa mujibu wa hati zao.
Washtakiwa hao wameondolewa na polisi kwa gari
ndogo binafsi, iliyozungukwa na umati mkubwa wa watu, wengi wao wakiwa
ni kina mama, ambao waliwazomea washtakiwa hao, na kusukuma gari yao
huku wakiikimbiza kuelekea kituo cha polisi, na kila mmoja akirusha
maneno ya kuwatuhumu washtakiwa hao.
Katika maelezo ya awali ya mashtaka, washtakiwa hao
wamedaiwa kula njama na kumfanyia ukatili mtoto huyo, ambaye mama yake
mzazi alifariki dunia na jukumu la malezi kuachiwa mama yake mkubwa
ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, kwa kumfungia kwenye boksi na kumyima
huduma za msingi, ikiwemo chakula, tiba, mavazi na malazi, hali
iliyosababisha apate ugonjwa wa nimonia,utapiamlo, maumivu ya kifua na
kuvunjika kwa mifupa ya miguu na mikono.
0 comments:
Chapisha Maoni