Jumatano, Juni 25, 2014

RELI YA KATI KUFUFULIWA

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, amesema Reli ya Kati itakuwa imefufuliwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu na kuanza kubeba mizigo itakayookoa barabara.
Akijibu hoja za wabunge kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali jana, Dk Mwakyembe alisema aliomba fedha za kununua vichwa na mabehewa ya treni na kukabidhiwa asilimia 90 ya fedha hizo, iliyobaki itatolewa wakati wowote.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, aliomba fedha ya vichwa 13 vya treni, akapewa na vitaingia Desemba mwaka huu na mabehewa 72 ya mizigo, ambayo yataingia Septemba mwaka huu.
Alisema pia mabehewa 22 ya abiria, fedha zake zilitolewa na Serikali na mabehewa 34 ya breki, ambayo yataingia kati ya Septemba na Agosti mwaka huu.
Fedha zingine zilizotolewa na malipo kufanyika kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ni za mabehewa 25 ya kokoto ambayo yataingia nchini miezi miwili ijayo ;na mashine ya kunyanyua mabehewa, ambayo nayo iko mbioni kufikishwa nchini.
Kutokana na uwekezaji huo, Dk Mwakyembe alisema Benki ya Dunia nayo imeamua kununua mabehewa 44 na vichwa vitatu vya treni, ili kuongeza nguvu katika jitihada hizo za kufufua reli ;na hivi karibuni na kuna vichwa vingine vitano, vinatengenezwa.

0 comments:

Chapisha Maoni