Jumatano, Juni 25, 2014

BENKI YA DUNIA YAIONYA SERIKALI YA TANZANIA JUU YA DENI LA TAIFA

BENKI ya Dunia imeonesha wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa deni la taifa kutokana na Serikali kuendelea kukopa mikopo ya biashara ya ndani hadi kuzidi kiwango kilichowekwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa asilimia 1.2 ya Pato Halisi la Taifa (GDP).

Hali ya uchumi wa Tanzania iliyotolewa jana na taasisi hiyo, imeonesha nchi imefanya vibaya zaidi katika maeneo ya mauzo ya nje, kushuka kwa nakisi ya fedha ya jumla, kushindwa kwa Serikali kukusanya mapato pamoja na ongezeko la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Ripoti hiyo iliyobatizwa jina la ‘Nani anataka kazi? Nguvu ya Mvutano wa Majiji’ imeeleza kuwa Tanzania imeonesha utendaji mbovu zaidi wa mauzo ya nje tangu mwisho wa miaka ya 1990.
Jambo lingine la kutia wasiwasi zaidi ambalo limetajwa na ripoti hiyo ni kwa nakisi ya fedha ya jumla kushuka hadi viwango vilivyo sawa na asilimia 6.8 ya GDP katika mwaka 2012/13.
Ripoti hiyo inasema huo ulikuwa ni upungufu mkubwa zaidi tangu mdororo wa uchumi wa dunia mwaka 2008/9. Katika eneo la mikopo, ripoti hiyo ilieleza kuwa thamani ya mikopo ilikuwa juu zaidi kwa asilimia 1.2 ya GDP kuliko lengo lililokubaliwa na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Mikopo hiyo ripoti inaeleza kuwa haikutosha kuziba pengo la fedha kutokana na deni kubwa la nyuma ambayo thamani yake ni karibu asilimia 4 ya GDP hadi ilipofika Juni 2013.
Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa robo za mwanzo za mwaka 2013/14 Serikali ilikusanya mapato yake kwa asilimia 82 tu ya lengo la mapato hali iliyosababisha Serikali kupunguza au kuahirisha utekelezaji wa baadhi ya programu za uwekezaji, manunuzi ya bidhaa na huduma.
Pamoja na kuchukuliwa hatua hizo, ripoti imebainisha kuwa thamani ya deni la taifa iliendelea kukua hadi kufikia karibu asilimia 5 ya GDP mwishoni mwa Machi 2014.

0 comments:

Chapisha Maoni