Ijumaa, Juni 13, 2014

MUHIMBILI HALI MBAYA, WAGONJWA KIBAO WANALALA CHINI

ZAIDI ya wagonjwa 40 waliolazwa katika wodi ya Sewa Haji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wanalala chini kwenye magodoro kutokana na ukosefu wa vitanda.
Hali hiyo imebainika baada ya wananchi na wagonjwa waliolazwa wodini hapo kutoa malalamiko yao na Tanzania Daima kushuhudia hali hiyo.
Tanzania Daima ilipofika wodini hapo, iliona wagonjwa hao wakiwa wamelala chini, huku wengine wakiwa wamelala kwenye korido kutokana na mlundikano wa wagonjwa.
Hatuelewi Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii bungeni anadai bajeti ya nini wakati Hospitali ya Taifa inatia aibu, haina vitanda wala vyandarua
alisema mmoja wa wananchi waliofika wodini hapo kuona wagonjwa wao.
Juhudi za kumtafuta msemaji wa hosptali hiyo kuzungumzia tatizo hilo, ziligonga mwamba baada ya kutokuwepo ofisini kwake na simu yake ya kiganjani kutopatikana.
Wakati huohuo, mlinzi wa wodi hiyo alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuwazuia watu waliofika hospitalini kuingia na maji na matunda na kudai muda huo (saa 6:30 mchana) ni wa chakula pekee, na kwamba muda wa kuleta matunda, juisi na maji ni saa 10 jioni.
Kutokana na hali hiyo, watu hao walianza kufanya vurugu na kuingia kuwaona wagonjwa wao huku wakidai kuna baadhi ya wagonjwa hawali chakula wanatumia juice na matunda.

0 comments:

Chapisha Maoni