Alhamisi, Juni 12, 2014

MANENO YA MBOWE KUHUSU BAJETI KUU

Akihojiwa na Kituo cha TBC baada ya kikao cha bunge jioni hii ambapo Serikali imewasilisha Taarifa yake ya Mwaka wa Fedha (bajeti kuu), Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni Freeman Mbowe amesema bajeti ya mwaka 2014/2015 kwa ujumla wake, haitoi nafuu yoyote kwa mwananchi.

Amesema kuwa Serikali inapoamua kuongeza vyanzo vya kodi kwa lengo la kupanua wigo wa mapato, inategemea imegusa maeneo gani, kwa sababu vyanzo vingine vilivyoongezwa mwaka ujao wa fedha vitaendelea kuongeza mzigo kwa mwananchi.
Kuhusu kuondoa au kupunguza misamaha ya kodi, KUB Mbowe amesema ni matokeo ya hoja za Kambi ya Upinzani Bungeni ambayo imepigia kelele suala hilo kwa zaidi ya miaka 2 sasa, lakini siku zote Serikali ilikuwa haitaki kutekeleza.
Hata hivyo amesisitiza kuwa Serikali ilipaswa kusema kwa misamaha ambayo imeondolewa au kupunguzwa, kiasi gani cha fedha kitaokolewa na kitaelekezwa kwenye matumizi gani.
Amesema inashangaza kuona kwamba Serikali bado imeendelea kutegemea kodi kwenye pombe, mvinyo, sigara etc.
Kuhusu suala la kodi ya PAYE, amesema kuwa punguzo la kutoka asilimia 13 hadi 12 bado ni kiwango ambacho kitawaumiza wafanyakazi nchini, akisema kuwa kwa muda mrefu sasa, Kambi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiitaka serikali kushusha hadi asilimia 9, jambo ambalo linawezekana.
Mjadala wa bajeti utaanza Jumatatu ijayo, ambapo Kambi ya Upinzani Bungeni itawasilisha bajeti mbadala pamoja na Taarifa ya Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2014/2015.

0 comments:

Chapisha Maoni