Mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa kivita,ICC
imesema kuwa imepata ushahidi wa kutosha kumfungulia mashitaka mbabe wa
kivita wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Bosco Ntaganda.
Ntaganda anashutumiwa kwa makosa ya Ubakaji,
mauaji na hata kuwasajili watoto wadogo kama wapiganaji wakati wa vita
vya mashariki mwa DRC.
Bosco Ntaganda, anayefahamika kwa
umaarufu zaidi kama Terminator, anakabiliwa sasa na mashitaka kumi na
nane ya uhalifu wa kivita, mauaji na pia kuwafanya watu watumwa katika
vita.
Mahakama hiyo ilipokea ushahidi wa zaidi ya
nyaraka elfu sitini na tisa kwa hivyo mwendesha mashtaka ameezelea imani
kuwa anayo kesi ya kutosha kumfungisha Ntaganda.
Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Bwana Ntaganda
alijisalimisha mwenyewe kwa ubalizo wa Marekani Mjini Kigali ambao
ulimpokea na kumkabidhi kwa mahakama ya ICC mjini The Hague.
Licha ya kuwa wanadai kupata ushahidi wa
kutosha, Mahakama hiyo sasa itakabiliwa na kibarua kigumu kubainisha
kuhusika moja kwa moja kwa bwana Ntaganda katika makosa wanayomshitaki
nayo.
Mawakili wanasema kuwa mauaji ya Uvira, mashariki mwa DRC yalilenga makabila ya Lendu, Bira na Nande.
Shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights
Watch limesema kuwa hatua ya kumfungulia mashitaka Bosco Ntaganda ni
hatua muhimu katika kuwalipizia haki waathiriwa wa mauaji ya DRC.
Wamesema pia kuwa huu ni ujumbe kwa wababe wa kivita kuwa hatimaye watakabiliwa na sheria kwa uhalifu dhidi ya binadamu.
0 comments:
Chapisha Maoni