Alhamisi, Mei 15, 2014

YALIYOJIRI KATIKA MKUTANO WA UKAWA IRINGA JANA JIONI

Watanzania wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata katiba mpya ikiwa ni pamoja na kuunga mkono hoja ya serikali tatu kama maoni yalivyo andikwa kwenye rasimu ya katiba iliyo wasilishwa na tume ya Jaji joseph warioba.
Akizungumza wakati alipokuwa akihutubia katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Mwembetogwa Manispaa ya Iringa,mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Profesa Ibrahimu Lipumba amesema kwa sasa watanzania wanahitaji kupata katiba itakayo linda rasilimali za nchi,kutetea na kulinda haki za binadamu,na itakayo wakata viongozi kuwa wawajibikaji.
Profesa Lipumba ameongeza kuwa walianzisha UKAWA baada ya kuona baadhi ya wanasiasa kutoka vyama vingine kutaka kuweka rasimu yao badala kujadili ile iliyowasilishwa na jaji warioba na kusaini na rais wa jamhuri ya muungano februari 22.
Naye mjumbe wa kamati kuu ya NCCR Mageuzi Bw: Banda Juju amesema kuwa ni vyema mawazo ya wananchi yaliyo kwenye rasimu ya katiba yakaheshimiwa na kulindwa ukilinganisha na gharama kubwa iliyotumika katika kukusanya maoni yao na wao wapo kukumbusha wajibu wa kila mtanzania katika taifa.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Iringa Mjini kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA) Mch. Peter Msigwa amesema Tanzania si taifa linaloongozwa kwa misingi ya kidini wa kabila,na wao watapita kila mahali kuwaambia wananchi kuunga mkono rasimu ya katiba iliyopelekwa na jaji warioba na si vinginevyo.
Hata hivyo kwa niaba ya jumuiya ya maimamu Tanzania sheik Rajabu Katimba amesema kukamilika kwa shughuli ya tume ya maoni ya katiba kumegharimu kiasi cha shilingi bilioni 60 na tume imefanya kazi kwa umakini,sasa kilicho tokea bungeni si kile kilicho kusudiwa kwani kukataa serikali tatu ni kupotosha jamii.

0 comments:

Chapisha Maoni