Jumanne, Mei 27, 2014

TAASISI YA SARATANI YA OCEAN ROAD KATIKA KASHFA MPYA, NI BAADA YA KUMNYANYAPAA MGONJWA ALIYEUZIWA DAWA FEKI ZA SARATANI YA TITI

Mgonjwa wa saratani ya titi aliyepewa dawa feki za mionzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) amejikuta katika wakati mgumu baada ya wahudumu wa hospitali hiyo ya Serikali kumtelekeza alipokwenda kupata tiba.
Mgonjwa huyo, Pendo Shoo ambaye anahofu kwamba saratani imempata katika titi lake la pili, anasema hatakwenda tena katika hospitali hiyo na badala yake ameamua kusaka tiba kwa waganga wa tiba asilia.
Hivi karibuni mtandao huu ulitoa habari kuhusu mtumishi wa OCRI, Almasi Matola alivyomtibu Pendo kwa dawa feki baada ya kumtoza kiasi cha Sh1.34 milioni kinyume na taratibu za tiba katika hospitali hiyo.
Almasi akizungumza na gazeti hili wiki mbili zilizopita, alikiri kuwekewa fedha katika akaunti yake ambazo ni zaidi ya Sh300,000, lakini akakanusha kwamba fedha hizo ni kama ujira wa kumpa mgonjwa huyo dawa.
Kwa mujibu wa taratibu za OCRI, wagonjwa wanaokwenda hospitali hapo kwa rufaa kutoka hospitali nyingine hawapaswi kutozwa fedha zozote kwa ajili ya matibabu. Pendo alipata rufaa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Novemba mwaka jana.
Alibaini kuwa alipewa dawa feki baada ya kutokupata nafuu yoyote wiki kadhaa tangu alipoanza kupewa tiba na baada ya kuripoti tukio hilo kwa madaktari walimwanzishia upya tiba husika.
Wiki moja tu baada ya kuchapishwa habari hizo, mgonjwa huyo alifika OCRI kuendelea na matibabu lakini alijikuta katika mazingira magumu kiasi cha kuondoka bila kupewa huduma.
Alisema Jumanne, Mei 20 mwaka huu, alikwenda OCRI kufuata majibu ya damu aliyokwishapeleka ili kujua iwapo saratani imesambaa katika titi lingine... 
Niliamua kurudi hospitali nikapime tena. Nilipofika kitengo cha kutoa damu nilitoa kwa ajili ya vipimo, lakini nilipokwenda tena kuchukua majibu walidai damu yangu imepotea. Kwa hiyo nililazimika kuanza upya, nilitoa damu tena na vipimo vyote vikawa tayari kama X-ray, Ultra sound na nikavipeleka kwa daktari.
Alisema alipatwa na hofu zaidi pale alipokwenda kwa daktari wake Dk Dominista Kombe ambaye alipaswa kumpa matokeo ya vipimo, lakini alishangaa pale daktari huyo alipomjibu kwa kusema: “Majibu yako utayajua hukohuko,” akimaanisha kwenye chumba cha tiba ya mionzi.

Chumba cha tiba

Alisema alipofika chumba cha tiba ya mionzi muuguzi aliyekuwapo alimwambia asubiri kwenye foleni hadi atakapoitwa jina lakini alikaa zaidi ya saa nzima bila faili lake kuitwa.
Alisema baadaye muuguzi alirudi na kumwambia aende nyumbani kwa sababu wagonjwa ni wengi. Lakini wagonjwa wengine waliokuwa kwenye foleni hawakupewa maelekezo hayo.
Kwa mazingira niliyoyaona, pale hospitali wameshaanza kuninyanyapaa kiasi kwamba naogopa. Kwa mfano, daktari niliyemtegemea anihudumie kwa upendo, juzi alinihudumia bila hata kuniangalia usoni, nilitegemea anipe majibu na ushauri hakufanya hivyo na kuniambia niende chumba cha chemo
alisema Pendo.
Dk Kombe kupitia simu yake ya kiganjani na baada ya kupokea kisha mwandishi kujitambulisha mazungumzo yalikuwa hivi:
Mwandishi: Haloo Dk Kombe…
Dk Kombe: Haloo, nani wewe?
Mwandishi: Ni mwandishi
Dk Kombe: Wale mliotuandika kwenye gazeti juzi?
Mwandishi: Ndiyo... (Baada ya majibu hayo, daktari huyo alikata simu na kila alipopigiwa hakupokea na baadaye simu yake ilizimwa kabisa).
Mkurugenzi wa Tiba wa OCRI, Dk Diwani Msemo alisema iwapo kuna wafanyakazi wanaonyanyapaa wagonjwa kama alivyodai Pendo, ni lazima uongozi wa hospitali ungechukua hatua.  
Huyo mgonjwa alikwenda kulalamika kwa uongozi wa hospitali? Kuna ofisi ya huduma za jamii, kuna Ofisi ya Mkurugenzi je, alikwenda?
alihoji Dk Msemo.

Alisema uongozi wa hospitali ungekuwa umegundua kama kuna unyanyapaa wa aina yoyote, basi waliofanya hivyo wangehojiwa na kuchukuliwa hatua na kwamba hatua hizo hutegemea kama mgonjwa ameripoti tatizo husika.
Kauli ya Dk Nsemo inatofautiana na ile iliyotolewa wiki mbili zilizopita na Mkurugenzi wa OCRI, Dk Twalib Ngoma ambaye alisema mgonjwa aliyefanyiwa vitendo hivyo anapaswa kwenda kushtaki kwenye vyombo vya sheria.
Anakuja kwako kulalamika wewe umsaidie nini, anatakiwa kwenda katika vyombo vya sheria ili apewe haki yake, wewe utamsaidiaje?
alihoji Dk Ngoma.

0 comments:

Chapisha Maoni