Kampuni ya Clouds Media International leo imetangaza kuwa imepewa
leseni ya kurusha matangazo katika nchi za umoja wa falme za kiarabu
(UAE). Akielezea kuhusu leseni hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni
hiyo Bwana Joseph Kusaga, amesema sasa kituo cha Clouds TV kimataifa
kitakuwa kikishuhudiwa na watu wa mataifa mbalimbali.
Clouds TV kimataifa ni mwendelezo wa televisheni maarufu sana kwa
vijana nchini Tanzania, hata hivyo sehemu kubwa ya maudhui
yatakayokuwemo kwenye Clouds TV kimataifa itakuwa na mpangilio mpana wa
vipindi kwa watazamaji vitakavyorushwa kwa lugha za Kiingereza na
Kifaransa. Akieleza zaidi Kusaga amesema
Leo ni siku ya kihistoria na alama ya hatua moja katika mpango wetu wa kina wa kupeleka maudhui ya Clouds TV kimataifa kupitia matangazo kwa njia ya mitandao.
Clouds TV kimataifa haitotoa tu burudani, lakini pia itakuwa
kiunganishi kwa waafrika waishio katika umoja wa nchi za falme za
kiarabu pamoja na kuwapa fursa za kutangaza bidhaa zao na kuimarisha
uhusiano baina yao.
Vituo vya televisheni katika Umoja wa falme za kiarabu vipo vingi na
vyenye ushindani mkubwa, lakini Clouds TV kimataifa imebahatika kupata
nafasi ya kurusha matangazo yatakayowafikia walengwa katika chaneli
yenye uwezo wa kuwahudumia zaidi ya watazamaji takribani milioni 3.5
kutoka katika nchi za Afrika. Kwa sasa hakuna kituo kinachotoa huduma
hii na hivyo kuwa fursa muhimu kwa watazamaji.
Clouds TV kimataifa itarusha vipindi vya burudani, tamthilia,
maigizo, ucheshi, na muziki, vyote vitakavyo kuwa vimeandaliwa kutoka
nchi za mashariki, magharibi na kusini mwa bara la afrika na itapatikana
kwa watazamaji walio katika Umoja wa falme za kiarabu kupitia huduma ya
IPTV inayotolewa na Etisalat na Du.
Clouds TV kimataifa itarushwa kupitia mamlaka ya Abu Dhabi
ijulikanayo kama twofour54, ikiungana na vituo kama FOX na CNN. Clouds
TV kimataifa itaanza kurusha matangazo ya majaribio katika wiki chache
zijazo kabla ya tarehe 15 mwezi June mwaka huu.
0 comments:
Chapisha Maoni