MBUNGE wa Nkasi, Ally Kessy (CCM), jana alinusurika kupata kipigo
kutoka kwa wabunge kutoka visiwani Zanzibar, baada ya kuwataka waache
kulalamika kila kukicha juu ya nafasi za uongozi.
Kessy aliwashambulia Wazanzibar, kwamba hawana sababu ya kulalamikia
kutaka haki sawa kwenye kila jambo la muungano wakati hawachangii kitu
kwenye Serikali ya Muungano.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo ndani ya Bunge, wakati akichangia hoja
ya hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Kessy alichangia hoja hiyo akijibu hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani
iliyosema kuna upendeleo mkubwa na uwiano usio sawa kati ya Tanzania
Bara na Visiwani katika uteuzi wa mabalozi wa Tanzania nje ya nchi.
Huku akiamsha hisia za ubaguzi wa muungano, Kessy, alisema kwa zaidi
ya miaka 20 Zanzibar, haichangii kitu katika Serikali ya Muungano,
lakini ndio vinara wa kulalamikia na kutaka usawa kwenye kila jambo.
Wakati akiendelea kuchangia hoja hiyo, Mbunge wa Chakechake, Mussa
Haji Kombo (CUF), aliomba mwongozo wa Naibu Spika dhidi ya kauli hiyo.
Mheshimiwa Spika, kuna mwendawazimu mwingine ni mtu anayepiga piga mawe hovyo, mwingine anakuwa mtu wa kuchekacheka, akipita anaweza kuwa anacheka tu ‘kwekwekwe’, na mwendwazimu mwingine ni yule anayeongea hovyo mbele ya watu wenye heshima zao kama tulivyo humu ndani.Wazanzibar sio watu masikini, wameingia kwenye muungano huu wenye watu milioni 45 kwa milioni 1.3. Hata kama mnatusaidia kama sadaka, basi hamtusaidii kitu.Ni aibu sana kwa mbunge wa CCM iliyotia saini na Zanzibar kuzungumza maneno hayo, Mheshimiwa Spika, naomba umwambie Kessy asiingie Zanzibar
alisema Kombo.
Akijibu taarifa hiyo, Kessy alikuja juu zaidi na kusema taarifa hiyo haikubali.
Mheshimiwa Spika, taarifa hii siikubali na kama anasema mimi mwendawazimu, yeye ndiye mwendawazimu zaidi, kwa hiyo naomba niendelee
alisema.
Kabla hajaendelea, Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, naye aliomba
kumpa taarifa Kessy kwamba kambi rasmi ya upinzani haijazungumzia suala
la majeshi Congo.
Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa mbunge kusema kundi la M23 ni Wanyarwanda na Waziri wa Ushirikiano wa Mambo ya Nje yupo na anapiga makofi
alisema.
Kama kawaida yake, wakati akijibu hoja hiyo, Kessy alisema anaijua
Rwanda kuliko Wenje anavyoijua, na anachokisema ni sahihi na ana uhakika
nacho.
Baada ya kauli hiyo, Bunge lilivurugika kwa takribani dakika tano kwa
wabunge kutoka Zanzibar kumtaka Kessy aombe radhi bila mafanikio.
Msimamo wa Kessy na maneno mengine aliyokuwa akiwashambulia
Wazanzibar, yaliibua mzozo mkubwa na kusababisha kutoelewana bungeni.
Naibu Spika alijaribu kuwatuliza bila mafanikio.
Hata hivyo, Ndugai, wakati akitoa mwongozo wa mzozo huo, alisema
tatizo lililopo ni kwamba wabunge wameamua kupeleka mada ya Bunge la
Samuel Sitta kwenye Bunge hilo na kuwataka wabunge wasubiri kujadili
mambo ya muungano kwenye Bunge la Katiba.
Nje ya Bunge
Baada ya kuahirisha Bunge, wabunge kutoka Zanzibar waliwahi kutoka nje kumkabili Kessy.
Mbunge wa Magogoni, Kombo Khamis Kombo, Sanya Mohammed Sanya na wabunge wengine wa CUF, walimzonga Kessy, kutaka kumpiga.
Kama si uwepo wa baadhi ya wabunge wa CCM walioamua kumuweka kati
Kessy, mbunge huyo angepigwa na wabunge kutoka Zanzibar ambao
walionyesha dhahiri kukerwa na kauli zake.
Alipoona mzozo umekuwa mkubwa na wabunge wa Zanzibar wanazidi kumjia
juu, Kessy, aliamua kutoka kwa haraka kwenda kwenye geti la kutokea huku
wabunge wenzake wa Bara wakimsindikiza na kuwazuia wale wa Zanzibar
kumfikia.
Baada ya Kessy kukimbia, Sanya, aliamua kumalizia hasira zake kwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano), Steven Wassira na kumhoji
kwanini wameshindwa kumdhibiti Kessy kutoa maneno ya kibaguzi dhidi ya
Wazanzibar.
0 comments:
Chapisha Maoni