Siku chache baada ya kifo cha mwongozaji na mwigizaji wa filamu Bongo,
Adam Philip Kuambiana, daktari mkubwa wa mastaa ameibuka na kudai
marehemu alijiua mwenyewe.
Kwa mujibu wa daktari huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe hapa
kutokana na maadili ya taaluma yao kuficha siri ya mgonjwa, siku moja
kabla ya kifo (Ijumaa ya Mei 16, mwaka huu), marehemu alimpigia simu na
kumwambia amekunywa dawa za malaria aina ya Fansidar lakini pia
amekunywa pombe.
Daktari huyo alieleza kuwa, marehemu alimpigia simu kumuomba ushauri
juu ya nini cha kufanya na kama kuna madhara yoyote juu ya pombe hizo na
dawa alizokunywa.
Aliniuliza kama kuna madhara yoyote ambayo anaweza kuyapata kwa kuwa alikuwa amekunywa fansidar kwa ajili ya malaria kisha akapata kiu ya bia na kuamua kunywa
alisema daktari huyo.
Akizidi kuzungumzia tukio hilo, daktari alikwenda mbele kwa kusema licha
ya msanii huyo kuwa na ‘masikhala’ mara kwa mara, lakini kwa kuwa
alimwambia jambo ambalo linahusu uhai wake, alimshauri kwenda hospitali
iliyo karibu ili akaonane na daktari kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa
kutoa sumu kwani kitaalam mtu anapokunywa pombe akiwa amemeza dawa za
aina hiyo vyote hugeuka kuwa sumu.
Alisema kutokana na jinsi alivyozidi kumsimulia hali aliyonayo,
aliamini kwamba marehemu alikuwa anamaanisha alichokuwa akikisema hivyo
ikabidi amsisitize kuwahi hospitali haraka.
Nilimwambia awahi hospitalini haraka kwani nilijua fansidar ni kali na si dawa ya kufanyia mchezo. Lakini kesho yake nilipopata taarifa za kifo chake niliumia sana japokuwa nilijua amejiua kwa kuchangaya fansidar na bia maana mchanganyiko wa sumu yake mwilini ni mkali sana
alisema daktari huyo huku akisisitiza kusitiriwa kwa jina lake.
Kwa mujibu wa mtu ambaye alikuwa karibu na Kuambiana siku ya tukio
ambaye naye hakutaka kutajwa jina gazetini, marehemu asingekufa ghafla
kama tatizo alilokuwa nalo lingekuwa la vidonda vya tumbo ambavyo
vilikuwa vikimsumbua kwa muda mrefu.
Siku ile marehemu alikuwa na pesa, alikunywa sana pombe kutoka asubuhi mpaka usiku mwingi, alikuwa anakula kila anapojisikia sasa hatuelewi ni kitu gani kilitokea maana haiwezekani mtu akutwe anaendesha na kutapika damu pasipo kuwa na sumu mwilini
alisema mtu huyo.
Katika hatua nyingine, daktari huyo aliwashauri mastaa wengine kuwa
makini kwani mara kadhaa amepata kesi za namna hiyo ambapo wanakunywa
pombe vilabuni usiku huku wakiwa katika dozi ya ugonjwa fulani.
Mimi nawaambia ndugu zangu, hasa mastaa waache tabia ya kunywa pombe wakiwa katika dozi, starehe zipo tu. Ni vyema wakawa wanauliza kwa wataalam wa afya pindi wanapokuwa wamemeza dawa za aina yoyote, nguvu ya dawa inatofautiana kulingana na ugonjwa husika na muda wa kukaa mwilini
alisema daktari huyo.
0 comments:
Chapisha Maoni