Mwandishi wa habari wa siku nyingi, Peter Temba amehukumiwa
kifungo cha miezi sita jela baada ya kushindwa kumpeleka mahakamani
mshtakiwa aliyemdhamini katika kesi ya kutorosha twiga kwenda Uarabuni.
Mwandishi huyo anayeandikia Gazeti la Serikali la
Daily News na mwenzake aliyekuwa akiandikia Gazeti la Nipashe, Jackson
Kimambo walimdhamini mtuhumiwa huyo raia wa Pakistan, Kamran Ahmed
ambaye ni mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro
ilitoa amri ya kuwakamata wadhamini hao baada ya mshtakiwa
waliyemdhamini kwa kutia saini hati ya dhamana ya maneno ya (bond) ya
Sh14.2 milioni, kutoroka.
Waandishi hao walimdhamini mshitakiwa huyo Juni
11, 2011 baada ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Moses Mzuna kuamuru
kila mshtakiwa akabidhi mahakamani Sh14.2 milioni au mali yenye thamani
hiyo.
Sharti la pili lilikuwa kila mshtakiwa katika kesi
hiyo ya kutorosha twiga wanne na wanyama wengine 148 kwenda Uarabuni,
kuwa na wadhamini wawili wakazi wa Kilimanjaro watakaosaini dhamana ya
Sh14.2 milioni kila mmoja na waliojitokeza ni waandishi hao.
Kesi hiyo ikiwa katika hatua za usikilizwaji,
Ahmed aliruka masharti ya dhamana na kwa miezi takriban mitano vyombo
vya dola vimekuwa vikimtafuta kwa udi na uvumba bila mafanikio na hata
wadhamini wake walishindwa kumpeleka mahakamani hadi ilipotolewa hati ya
kuwakamata.
Temba alikamatwa Jumatatu wiki hii na kufikishwa
mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Mfawidhi, Simon Kobelo na
alipoulizwa alipo mshtakiwa huyo alisema hajui na hana Sh14.2 milioni
alizosaini kama dhamana.
Wakili wa Serikali, Stella Majaliwa aliomba sheria
ichukue mkondo wake kwa kuwa mshtakiwa katika kesi hiyo pamoja na
mdhamini wa pili hawajulikani walipo.
Kobelo alisema sheria iko wazi na kwamba kulingana
na Kifungu cha 160(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA),
kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mdhamini huyo atatumikia
kifungo cha miezi sita jela.
Kufungwa kwa mwandishi huyo kumeibua simanzi kubwa
miongoni mwa wanahabari na familia yake hasa ikizingatiwa kuwa ni mwaka
jana tu, alikatwa mguu mmoja kutokana na maradhi ya kisukari.
0 comments:
Chapisha Maoni