Baadhi ya wafanyabiashara wamesema
vikwazo vya ndani vya kufanya biashara vinawakatisha tamaa ya
kuchangamkia masoko kwenye nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC).
Wafanyabishara hao walisema hayo hivi karibuni
kwenye kongamano la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoandaliwa na Wizara
ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Wakichangia katika kongamano hilo, wafanyabishara
hao walisema bado kuna vizuizi vingi kwenye barabara ambavyo
vinawasababishia usumbufu mkubwa.
“Bado barabara zetu zina vizuizi vingi, kuna aina
nyingi za ushuru unaokatisha tamaa wafanyabiashara,” alisema Shaaban
Saleh (34) mkazi wa Chakechake, Pemba .
Aliongeza kuwa: “Viongozi wanatuhamasisha
kuchangamkia soko la nchi za Afrika Mashariki wakati hapa nyumbani
hakuna mazingira mazuri ya kufanya biashara, tutavukaje kwenda uko.”
Naye Mkazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Omar
Suleiman Ali (51), alisema yeye ni mtengenezaji wa viungo, lakini
imekuwa tabu hata kuvifikisha kwenye maonyesho ya sabasaba Viwanja vya
Mwalimu Julius Nyerere.
“Ukitoka Zanzibar ukifika katika Bandari ya Dar es
Salaam unasumbuliwa, wanafanya ukaguzi utadhani unaingia katika nchi
nyingine wakati sisi tayari tuko katika muungano,” alisema Ali.
Alisema bidhaa anazozitengeneza zimekosa alama za
viwango vya ubora kwa sababu Zanzibar hakukuwa na taasisi kama ilivyo
Shirika la Viwango vya Ubora (TBS) kwa upande wa Tanzania Bara. Alisema
kikwazo hicho kilikwamisha uuzaji wa bidhaa zao kwa sababu wanunuzi
wanataka kufahamu ubora wa bidhaa.
0 comments:
Chapisha Maoni