Chama cha Wavuvi Tanzania (Taf) kimesema hali ya upatikanaji
samaki kwenye Ziwa Victoria imeshuka kwa kasi kutokana na kuongezeka kwa
vitendo vya uvuvi haramu.
Pia, Taf kimesema sheria za uvuvi zinawabana
wavuvi wadogo kupata faida na badala yake zinatoa nguvu kwa viwanda
vikubwa vya samaki, jambo ambalo alisema linachangia kupunguza ajira kwa
vijana mkoani hapa.
Wakizungumza juzi kwa nyakati tofauti kwenye Soko
la Samaki Mwaloni, mwenyekiti wa Kamati ya Fedha wa Taf, Bakari Kadabi
alisema upatikanaji samaki umeshuka kwa kiwango kikubwa kutokana na
kuongezeka kwa vitendo vya uvuzi haramu na mapambano hayajafanikiwa.
Alisema asilimia 70 ya uchumi wa Mwanza inategemea uvuvi, hivyo upungufu huo unashusha mapato ya Serikali.
“Kwa miaka miwili upatikanaji wa samaki Ziwa
Victoria umepungua kwa kasi kutokana na uvuvi haramu kuongezeka. Hali
hiyo inasababisha mazalia ya samaki kuharibika,” alisema Kadabi.
Kadabi alisema watu milioni tatu wanategemea uvuvi
kupata kipato, tofauti na sekta ya viwanda ambayo inachukua watu
300,000, hivyo ni vyema Serikali ikaweka mikakati sahihi ya kupambana na
uvuvi haramu Ziwa Victoria.
Naye katibu wa wauza samaki sokoni hapo, Edina
Tibanga alisema soko la samaki limetekwa na wafanyabiashara wa kigeni,
kitu ambacho kinawanyima fursa kunufaika na biashara hiyo. “Hapa sokoni
wengi ni wafanyabiashara wa kigeni hasa kutoka nchi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku Watanzania wakibakia kuwa vibarua.
Haturidhishwi na hali hiyo,” alisema Tibanga.
0 comments:
Chapisha Maoni