Wapo wanaoombea msimu wa mvua uanze ili hali ya joto la Dar es
Salaam ipungue, lakini kwa wakazi wengi huwa na maombi tofauti na wakati
mwingine wingu jeusi linapotanda tu, taratibu za kuhama makazi yao
huanza.
Ni maisha ya mguu ndani mguu nje. Katika maeneo
mengi ukipita utaona magodoro na samani nyingine zimeanikwa nje au
kuhifadhiwa juu ya paa.
Wanaoishi maeneo ya mabondeni huogopa kulala ndani
wakihofu huenda wakasombwa na maji wakati wowote kwa kuwa hata kama
mvua hazinyeshi kwenye maeneo yao, bado hufuatwa na maji kutoka maeneo
mengine ambako mvua hunyesha.
Katika miaka ya karibuni mvua kidogo tu imekuwa
ikisababisha kadhia mbalimbali kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam,
ikiwemo mafuriko na ongezeko la msongamano wa magari barabarani.
Ongezeko la watu, kuziba kwa mifereji ya kupitisha
maji na kujenga katika njia za maji ni baadhi ya sababu zinazotajwa
kuchangia kuwafanya wakazi wa Dar es Salaam hasa waishio mabondeni,
kukosa usingizi katika kipindi hiki.
Gazeti hili lilifika katika baadhi ya maeneo na
kushuhudia familia zikiwa nje ya nyumba zao. Wengine wakiwa wamefungia
vitu vyao ndani na kuelekea maeneo mengine wakisubiri maji yakauke ili
warudi kuendelea na maisha mabondeni.
Maisha kipindi cha mvua
“Hivi sasa tunaishi kwa machale. Tukiona wingu au
mvua imeanza kunyesha tunaondoka. Mali inaweza kutafutwa lakini sio uhai
wa mtu,” anasema Madande Jabir mkazi wa Gongo la Mboto.
Jabir anasema mvua ya saa mbili iliyonyesha juzi
katika maeneo hayo imesababisha maafa makubwa, ikiwemo kubomoa kuta za
nyuma, kuharibu samani na mazao yaliyokuwa shambani.
“Kama isingekuwa machale, ina maana ile nyumba
ilipobomoka ingeua watu, lakini tunaishi kwa kujihami na kujibanza
popote salama unapoona mvua haiwezi kukubeba,” anasema Jabir.
Wakazi wa Nyaishozi nao wanastaili nyingine ya maisha ambao inasababishwa na maji kujaa ndani ya nyumba zao.
Mwanahamisi Juma anasema maji yameingia mpaka
ndani, lakini kwa kuwa si mengi sana, wanalazimika kuendelea na maisha
ingawa hali hiyo ina hatarisha afya zao.
0 comments:
Chapisha Maoni