Alhamisi, Aprili 10, 2014

SUALA LA SERIKALI MBILI NA SERIKALI TATU BADO LINALETA MZOZO, TAZAMA VIDEO

Huku suala la muundo wa Muungano likizidi kuligawa Bunge Maalum la Katiba, wajumbe wa Kamati mbalimbali za Bunge hilo wanaowakilisha Walio Wachache wameonekana kuunga mkono serikali tatu huku wale wanaowakilisha Walio Wengi wakiupinga. 
Mwakilishi wa Maoni ya Wachache toka Kamati No. 5 ya Bunge hilo Maalum, David Kafulila, amesisitiza kuwa serikali ya Muungano iliyopendekezwa na Rasimu ya Pili ya Katiba yaweza kujiendesha kwa kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato.
Kwa mfano, mapato ya ushuru wa bidhaa bandarini yanaweza kutumiwa vyema kuiendesha serikali hiyo itakayofanya kazi kwa kuzingatia mfumo wa serikali tatu: Uamuzi ambao Mh. Kafulila anaamini utajenga misingi imara ya uendeshaji wa serikali.
Hata hivyo, katika ripoti yake iliyowakilisha maoni ya Walio Wengi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Assumpter Mshama amedai kuwa mfumo wa kiutawala wa serikali 3 utadhoofisha Muungano.
Hoja hiyo imeakisiwa katika ripoti iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati No. 2, Shamsi Vuai Nahodha, aliyedai kuwa wajumbe wa Kamati yake wameukataa mfumo wa Shirikisho La Serikali Tatu wakisema unahatarisha usalama wa nchi wanachama.
Lakini mtazamo huo umepingwa na mjumbe aliyewakilisha Walio Wachache kwenye Kamati hiyo, Emmanuel Makaidi, aliyebainisha kuwa mfumo wa Serikali 3 utasaidia kukuza demokrasia, ambayo ndiyo kiini cha maendeleo ya nchi yoyote duniani.

0 comments:

Chapisha Maoni