Wakizungumza na mwandishi wetu jana, baadhi ya
wajumbe wa Bunge hilo, ambao wapo katika kundi la wachache, walisema
wenyeviti hao, ambao wengi wao ni viongozi wa CCM, wamegoma kuzipokea
taarifa zao ambazo walipewa wazisome leo bungeni.
Mwenyekiti wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
Freeman Mbowe alisema kuwa, mgogoro huo umeibuka kutokana na wajumbe wa
Bunge hilo, ambao wengi wao wanatoka CCM, kupuuza hoja ya awali ya
kutaka maoni ya walio wachache wayasome wenyewe bungeni, badala yake
wakalazimisha yasomwe na wenyeviti wa kamati wanaotoka kwenye kundi la
walio wengi.
“Wameshtuka walipoziona hoja zetu, hawakutarajia
hoja za walio wachache, kwani wao hawasomi kanuni na hoja zao, nyingi
wamekaririshwa, hivyo hawawezi kuzitetea,” alisema Mbowe. Alisema hadi
jana jioni kwenye kamati yake, kulikuwa na mgogoro juu ya maoni ya walio
wachache kama ilivyokuwa kwenye kamati nyingine.
Mjumbe wa Ukawa, Tundu Lissu alisema kamwe
hawatakubali taarifa za walio wachache kupunguzwa maneno na wenyeviti wa
kamati kwani maoni hayo siyo yao, ni ya wengine.
“Hizi taarifa ni zetu hatutakubali waondoe hata
neno moja, waling’ang’ania kuzisoma sasa lazima wasome maneno yote kama
kanuni inavyosema, wakipuuza kesho (leo) bungeni hatutakubali,” alisema
Lissu.
Mmoja wa wenyeviti wa kamati hizo, Paul Kimili
alikiri kuwa katika kamati yake Namba 12, aliomba taarifa ya walio
wachache kuandikwa kwa kufuata utaratibu na kupunguza lugha ambazo
alisema siyo nzuri.
“Ni kweli kuna mgogoro, hizi taarifa za wachache
kuna maneno mengine makali sana ya kuudhi, sasa kwangu nimewaomba
warekebishe tu,” alisema Kimiti.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis
Michael naye alisema amewataka wajumbe wa kamati ya walio wachache
kurekebisha taarifa yao, baada kuandika maneno ambayo yanahitaji
ushahidi.
Huu uamuzi wa kuwataka warekebishe baadhi ya
maneno siyo wangu, ni wa Kamati. Kwanza ni mjumbe gani analalamika?
Kanuni zipo wazi anayepaswa kuzungumza na vyombo vya habari ni
mwenyekiti pekee na mjumbe mwingine akitaka kuzungumza lazima apate
idhini ya mwenyekiti,” alisema Dk Michael. Mwenyekiti wa Kamati Namba 9,
Kidawa Hamis na Mwenyekiti wa Kamati Namba tano, Hamad Rashid ambao
jana mchana walikabidhi taarifa za kamati zao kwa Makamu Mwenyekiti wa
Bunge Maalumu, Samia Suluhu Hassan walisema kuwa katika kamati zao
washauriana vizuri na hakuna mgogoro.
“Mimi kamati yangu tulikaa na kujadiliana na
wachache wana taarifa yao na wengi wanayo ya pamoja, tatizo ambalo
lilikuwapo, utakuta wachache wameandika maneno mengi zaidi ya kurasa 50
na walio wengi wana maneno machache, hivyo hapo lazima kufikia
maridhiano,” alisema Hamis.
Hata hivyo, Suluhu, alisema hadi jana, alikuwa hajapokea malalamiko ya kamati yoyote ya maoni ya walio wachache kukataliwa.
0 comments:
Chapisha Maoni