Jumamosi, Aprili 19, 2014

FAHAMU MADHARA YA KUFANYA KAZI NA WANAWAKE WAREMBO KATIKA OFISI MOJA

Kufanya kazi sehemu moja au kuzungumza na mwanamke mwenye mvuto kunaweza kumfanya mwanaume apoteze umakini wake, hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la New Study.
Wanaume wanaofanya kazi kwenye makampuni yenye ‘visura’ wengi, ufanisi wao ni wa kiwango cha chini kulinganisha na wasiokuwa kwenye mazingira hayo, sehemu ya utafiti inaeleza.
Sababu ya kuwepo kwa hali hiyo ni uchunguzi kubaini kuwa, akili za wanaume wenye kuvutwa na sura wakati wakifanya mambo hukabiliwa na mgongano wa hisia mbili, za kazi na mapenzi.
Kuwepo kwa vitu hivyo viwili kwa wakati mmoja ndani ya akili ya mwanaume, utafiti wa kitaalamu uliochapishwa na Jarida la Journal of Experimental and Social Psychology, umebaini kuwa mwanaume ana hatari kubwa ya kufanya vibaya kikazi kwa sababu wakati akifanya kazi yake atakuwa pia akifanya kaziya kushawishi au kuimarisha hadhi yake mbele ya mwanamke aliyemvutia.
Ukichunguza, utabaini kuwa, tabia za wanaume (si wote) hubadilika pindi wanapokuwa mbele ya wanawake warembo, hii ikiwa na maana kuwa, kama mwanaume ni mwenye maneno mengi na mpayukaji kwa mfano, hujikuta akilazimika kushusha sauti yake, kuongea kwa unyeyekevu na busara lengo ni kutaka kumvutia msichana.
Hali hiyo inapojitokeza ndiyo inayotajwa kudhorotesha umakini wa mtu na kumfanya afanye kazi zake kama ‘msanii’ anayeigiza na hivyo kuathiri utendakazi wake.
Wakati nafanya uchunguzi wangu kwa kuoanisha na ule wa watafiti wengine wa kimatafa ukiwemo wa Dr. Irva Hertz-Picciotto, kutoka Chuo cha Carifonia Marekani, nilibaini pia viashiria vingine vya ufanisi duni wa kimasomo kutoka shule za jinsia moja na zile za mchanganyiko, ambapo uchunguzi unaonyesha kuwa wavulana wanaosoma shule huku wakiwa na uhusiano wa karibu na wasichana warembo huathirika kisaikolojia.
Hata hivyo, upo ushahidi mwingine kwamba kiwango cha kufaulu cha shule mchanganyiko kuwa chini kuliko wa shule za wasichana au wavulana peke yao, katika kulithibitisha hili mazingira ya shule na malezi yanazingatiwa.
Katika kumbukumbu iliyowashangaza wanasaikolojia na watafiti wa chuo cha Radboud cha Netherland ni pale mmoja wao aliposhindwa kukumbuka na kumwelekeza msichana mwenye mvuto aliyekutanishwa naye ramani ya eneo analoishi, jambo ambalo wenzake walisema lilitokea kwa sababu alikuwa kwenye mhemko wa hisia za kimapenzi.

Utafiti wao huo ulihusisha pia watu wengine na matokeo yalionyesha udhaifu mwingi kwa wanaume, huku wanawake wakiwa na kiwango kidogo cha kuathirika kwa kukutanishwa na wavulana wenye mvuto.
Ingawa si jambo la hatari sana kufikia hatua ya kulitangaza moja kwa moja kuwa ushirikishwaji wa wanaume na wanawake warembo katika ofisi, masomo na kazi mbali mbali una madhara lakini kitaalamu imebainika kuwa ni vema kundi linaloathirika ambalo ni sawa na asilimia 19 ya wanaume wote likapewa elimu ili kupunguza zaidi madhara ya kisaikolojia.
Changamoto hii, inamtaka kila mwanaume kupima mwenyewe mhemko wa nguvu za warembo kwa kujiuliza maswali ambayo yatamuwezesha kujua kama yuko kwenye kundi la wanaume wanaoweza kuathirika kisaikolojia kwa kufanya kazi na wanawake wenye mvuto au la! Lengo likiwa ni kuchukua hatua za kujikinga na madhara ya kisaikolojia.
Mwanasaikolojia Dr George Fieldman anakumbusha kitu muhimu alichokipa jina la ‘Reproductively Focused’ kuwa ndiyo sumu kali inayowadhuru wanaume wengi wanapokutana au kukutanishwa na wanawake wenye mvuto. Inaelezwa kuwa wanaume wanaovamiwa haraka na hisia za kimapenzi ndiyo wanaoweza kupata madhara ninayoyaeleza kwa kiwango kikubwa.
Zipo njia nyingi za kitaalamu za kupima ili kubaini kuwa mwanaume anakabiliwa na tatizo hili au la! Lakini pamoja nazo ni hii ya kujibu maswali, ambayo imeonekana kuwa ni rahisi zaidi kwani haihitaji mtaalamu wa kumuongoza mhusika bali ni kwa mtu mwenyewe kutafakari na kupata majibu kama urembo wa mwanamke unaweza kumuathiri kiutendaji. Maswali ya kujiuliza ni haya:
>>Je una uwezo wa kuongea na mwanamke bila kushika shika vitu? Kwa mfano kuingiza mikono mfukoni, kuchezea simu, kalamu au hata kujipapasa mwenyewe.
>>Je Unaweza kutazamana naye usoni kwa zaidi ya sekunde 36 bila kuona aibu? Unaweza kutembea hatua nne mbele ya mwanamke bila kuhisi mwili wako ni mzito?
>>Je unajiamini unapokuwa na mazungumzo na mwanamke hasa mkiwa wawili tu, au mpaka uwe na mtu mwingine?
>>Je umewahi kuwa na ukaribu na wanawake warembo wangapi na kati yao ni wangapi uliwatongoza?

Baada ya kujiuza maswali hayo sahihisha kulingana na majibu yako. Endapo utakosa yote fahamu kuwa wewe ni miongoni mwa watu wanaoweza kupata athari ukipewa nafasi ya kufanya kazi na wanawake warembo. Kumbuka kuwa jibu la mwisho lazima idadi yake isizidi nusu, endapo umewahi kuwa na urafiki wa karibu na wanawake warembo 10 kwa mfano na kati ya hao watano au zaidi uliwatongoza, utambue kuwa unaviashiria vibaya vya kupata
madhara tunayoyazungumza.
Ifahamike pia kwamba watu wanaotafunwa na ‘virusi’ hivyo vinavyoletwa na mvuto wa wanawake warembo ndiyo hao ambao hutumia vyeo au nafasi zao vibaya kwa kuajiri au kutoa nafasi za
upendeleo kazini kwa wanawake wasiokuwa na sifa za kufanya kazi husika na hivyo kujikuta ofisi, wizara na hata biashara zinakosa tija.
Wakati nafanya uchunguzi kuhusu tatizo la kushirikiana kikazi na wanawake warembo ambapo niliwahoji baadhi wanafunzi, wafanyakazi na wafanyabiashara maswali niliyoandika hapo juu, wengi walibainika kuwa na tatizo hili, hata hivyo changamoto iliyokuwepo ni juu ya swali lao la msingi kwamba wafanye nini wasiathiriliwe kisaikolojia baada ya kuwepo kwa dalili za tatizo?
Jibu la swali hili ni dogo nalo ni kujitambua na kuwa makini.
Inashauriwa kuwa watu wenye matatizo haya wanatakiwa kudhibiti mawazo yao ya kimapenzi mara wakutanapo na wanawake warembo na kusimamia vitu halisi. Jambo la mwisho ni kujiamini na kutenda yale wanayofahamu.
Katika hali ya kawaida tatizo la mvuto wa wanawake hugusa zaidi hisia, hivyo mara nyingine ni vigumu kwa mtu kuweza kuzuia msukumo usitokee, lakini kwa aliyejitambua itakuwa rahisi kwake kutoendeleza mawazo ya kimapenzi sambamba na kazi.
Wakati mwingine ni suala la mtu mwenyewe kuamua kusimamia kazi na kupuuza hisia za kimapenzi zilizotokana na mvuto wa mwanamke mrembo, kwa vile si lazima kila mawazo au hisia zinazotokea ziendelezwe.
Hebu tujiulize ni mara ngapi huwa tunawaza au kuhisi vibaya na tukaacha kufanya kama tulivyofikiri kabla? Je hakuna vipindi ambavyo huwa tunawaza kuua, kuacha wake zetu na hata kufanya mapenzi na ndugu na mambo mabaya kama hayo na tukayapuuza mawazo hayo? Ikiwa tumeshafanya hivyo tufahamu kuwa nguvu kubwa iko kwenye uamuzi wetu.
Nikimalizia somo hili ni kwamba, mara nyingi wanaume wenye aibu na hofu mbele ya wanawake ni wale wanaodhani kuwa wanakasoro fulani ambazo zinaweza kuwakosesha penzi na hivyo kuamua kujikarabati kwa unyenyekevu, sauti za chini, hongo, kutembea kwa madaha na wakati mwingine kujifanya ni watu wa tofauti sana kwenye jamii, jambo ambalo huweza kuathiri mwenendo wao na kuwa watu wa kuigiza igiza mambo yasiyoendana na uwezo wao halisi au kile wanachokifahamu.
Nimalizie mada hii kwa kufafanua kuwa lengo la makala haya si kuzuia ushirika kati ya wanaume na wanawake warembo bali kufundisha watu kuhusu madhara yake ili ukiwapo urafiki uwe ni ule wenye tija, usioathiri ufanisi wa kazi.

0 comments:

Chapisha Maoni