Jumatano, Aprili 30, 2014

ASKARI POLISI WAWILI WAUAWA URAMBO TABORA KATIKA TUKIO LA UJAMBAZI

ASKARI Polisi wawili kutoka Tarafa ya Usoke wilayani Urambo mkoani Tabora, wameuawa kwa kupigwa risasi na majambazi. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda, alisema mauaji hayo yamefanyika juzi saa 2: 30 usiku katika kijiji cha Usoke wilayani rambo. Kamanda Kaganda aliwataja askari waliouawa kuwa ni PC Shabani, mwenye namba G 3388 ambaye alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi na majambazi hao.
Mwingine ni PC Jumanne mwenye namba F.5179, aliyejeruhiwa tumboni na baadaye kufa jana saa 4 asubuhi, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Akisimulia zaidi tukio hilo, Kamanda huyo alisema majambazi hao walikuwa watatu na kabla ya mauaji hayo, walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara Ibrahim Mohamed, ambaye ni mkazi wa Usoke na kupora fedha taslimu Sh 1,200,000.
Mbali na uporaji wa fedha, pia walipora vocha za simu aina mbalimbali zenye thamani ya Sh 120,000 ambapo baada ya askari hao kupata taarifa ya uhalifu huo, walienda eneo la tukio kutoa msaada zaidi.
Kamanda huyo wa Polisi, alifafanua kuwa askari hao wakiwa mita chache kabla ya kufika katika eneo la tukio, walikutana na majambazi hao na kuanza kuwafyatulia risasi kwa kasi na kumuua PC Shaabani.

Ndugu zangu waandishi wa habari hili ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la Polisi, lakini naapa kuwasaka hadi kuwakamata wakiwa hai au wafu...tumechoka na uhalifu huu
 alisema Kaganda.
Kamanda Kaganda alisema kabla ya mauaji ya askari hao, majambazi hao walifyatua risasi hovyo hewani kwa lengo la kuwatisha raia ambapo maganda 25 ya risasi aina ya SMG na SAR yameokotwa katika eneo la tukio.
Kutokana na mauaji hayo, Polisi mkoani Tabora wanaendesha msako mkali usiku na mchana, ambapo tayari hadi sasa watu watano wametiwa mbaroni na Polisi wakituhumiwa kuhusika na mauaji hayo.
Kamanda Kaganda alitoa mwito kwa wananchi mkoani Tabora, kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kuwabaini majambazi hao.
Akizungumzia mauaji hayo jana katika ofisi za Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alitoa pole kwa wananchi wote waliofiwa na ndugu zao.
Alisema Jeshi la Polisi limeanzisha msako mkali wa majambazi hao ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

0 comments:

Chapisha Maoni