Alhamisi, Januari 30, 2014

JUSTIN BIEBER AMTWANGA DEREVA

MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa Pop kutoka Canada, Justin Bieber amefunguliwa mashtaka kwa kumpiga dereva wa gari la kifahari la kukodisha mwezi Desemba mwaka jana.

Bieber mwenye umri wa miaka 19 alikaribishwa katika kituo cha polisi cha Toronto na kikosi kikubwa cha wapiga picha za televisheni pamoja na mashabiki wake.
Amefunguliwa mashtaka ikiwa ni ndani ya wiki moja baada ya kukamatwa mjini Florida Marekani kwa shutuma za kuendesha gari akiwa amelewa.
Mwanasheria anayesimamia kesi ya mwanamuziki huyo kutoka Marekani amesema mteja wake hana makosa.
Kwa mujibu wa polisi wa Toronto, yapata saa 2:50 saa za Canada tarehe 30 Desemba mwaka jana, gari la kifahari liliwasili kumchukuwa Bieber na wenzake watano katika klabu moja ya starehe ili kuwarejesha katika chumba chao cha hoteli.
Wakati wakiwa njiani, dereva huyo pamoja na mmoja wa abiria wake, aliyetajwa kuwa Bieber, walianza kufokeana na kutoleana maneno makali.Abiria
huyo "alimgonga dereva huyo kwenye kisogo mara kadhaa", polisi wamesema.

Dereva huyo inasemekana alisimamisha gari lake na kisha kutoka nje na kuwaita polisi japo Bieber alifanikiwa kutokomea kabla ya polisi kufika eneo hilo.

Bieber alijisalimisha polisi Jumatano na anatarajiwa kufikishwa kizimbani Machi 10, 2014.
Howard Weitzman, wakili wa Bieber mjini California, amesema msanii huyo hana hatia na kwamba anatarajia kesi hiyo itachukuliwa kama kosa dogo tu.
Justin Beiber amejikuta matatani mara kadhaa na maafisa wa polisi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Mapema asubuhi Alhamisi iliyopita, Bieber alikamatwa kwenye ufukwe wa Miami baada ya ofisa mmoja wa polisi kumfumania akiendesha kwa kasi gari la kukodi aina ya Lamborghini rangi ya njano kwenye barabara ya umma.
Akimshuku kuwa alikuwa mlevi afisa huyo alimtia mbaroni.
Kadhalika alifunguliwa mashtaka ya kupinga kukamatwa na pia kuendesha gari akiwa na leseni iliyopita muda wa matumizi.

0 comments:

Chapisha Maoni