Ndege zisizo na rubani za Marekani zimeuwa kwa akali watu
2,400 duniani katika kipindi cha miaka mitano tokea Rais Barack Obama
aingie madarakani nchini humo.
Uchunguzi uliofanywa na Bureau of Investigative Journalism (TBIJ)
yenye makao yake nchini Uingereza unaonyesha kuwa, kuanzia mwaka 2009
yamefanyika karibu mashambulio 390 ya ndege zisizo na rubani katika nchi
za Pakistan, Yemen na Somalia, kiwango hicho kikiwa ni mara nane ya
mashambulio yaliyofanywa katika kipindi cha uongozi wa George W. Bush
Rais wa zamani wa Marekani. Ripoti ya TBIJ imeonyesha kuwa, nchini
Pakistan pekee kuanzia mwaka 2009 hadi sasa, jumla ya watu 951
wameshauawa wakiwemo watoto 200. Ripoti hiyo imeeleza kuwa, drone za
Kimarekani zimefanya mashambulio 58 nchini Yemen na kuuwa zaidi ya watu
281. Inafaa kuashiria hapa kuwa, mwezi Oktoba mwaka jana Shirika la
Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilikosoa vikali
mashambulizi yanayofanywa na ndege zisizo na rubani za Marekani katika
nchi mbalimbali, na kutaka ufanyike uchunguzi wa mauaji dhidi ya wahanga
ambao hawana mafungamano yoyote na makundi ya kigaidi.
0 comments:
Chapisha Maoni