Jumapili, Januari 26, 2014

MBIO ZA JENISTER MHAGAMA KUIPAISHA ELIMU YA TANZANIA KUISHIA UKINGONI? HII NDIO KASI ALIYOANZA NAYO

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Muhagama, ameitaka  Taasisi ya Elimu ya Taifa  (TET) kuweka uzalendo kwa kuangalia upya tatizo la mitaala ya elimu  ili iwe ya viwango vinavyokubalika.
Akizungumza wakati azinduzi wa  Baraza la TET ambalo ni kama bodi ya wakurugenzi jijini Dar es salaam jana, Mhagama, alisema kukiwa na uwajibikaji katika utendaji wa kazi malalamiko ya  wananchi yatapungua.
Alisema wakati wa taasisi hiyo kufanya mambo  kwa kificho umekwisha, badala yake viongozi na wafanyakazi waanze wachape kazi kwa uwazi na weledi utakaoleta mafanikio  haraka.
Naibu waziri huyo, alilitaka baraza hilo kusimamia kazi ya uinuaji  elimu kulingana na mpango wa matokeo makubwa sasa kwa kutafuta njia ya kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia mashuleni.
“Muda wa kukaa ofisini umekwisha, kuna malalamiko mengi kutoka wananchi ambayo yanahitaji majibu, nendeni huko mkawaeleze mitaala ya elimu mliyutunga ipo mingapi kuliko mnawaacha watu wanasema watakavyo,’ alisema Mhagama.
Alisisitiza kuwamba baraza  hilo linawajibika kwa Waziri wa Elimu, hivyo lina wajibu wa kumshauri kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya sekta hiyo.
Mwenyekiti wa Baraza ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Profesa Idrisa Kikula atakayeshirikiana na wajumbe wengine wanane na kufanyakazi kwa miaka minne.

Akitoa shukrani zake kwa Naibu waziri, Profesa Kikula, alisema baraza lake litahakikisha linafanya kazi  kwa kufuata sheria na kanuni ikiwamo kusimamia mitaala inayotungwa.
“Nakuhakikishia Naibu waziri sisi tupo macho kama mitaala mibaya tutasema hapana, tukifanya kinyume chake tutakuwa hatuwatendei haki wananchi waliotukabidhi majukumu haya,” alisema.

0 comments:

Chapisha Maoni