Jumapili, Mei 14, 2017

KIPINDUPINDU CHAUA 115 KWA SIKU 17 YEMEN

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu imesema mlipuko wa kipindupindu nchini Yemen umesababisha vifo vya watu 115 hususan watoto wadogo katika kipindi cha siku 17 zilizopita.
Akihutubia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Yemen, Sana'a jana Jumapili, Dominik Stillhart, Mkurugenzi wa Operesheni wa Msalaba Mwekundu amesema vifo hivyo vilitokea kati ya Aprili 27 na Mei 13.
Afisa huyo wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ameongeza kuwa, kesi 8,500 za ugonjwa huo zimeripotiwa kufikia sasa katika majimbo 14 ya nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Wakati huo huo, Sherine Varkey, Naibu Mwakilishi wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF nchini Yemen amesema hospitali chache zilizosalia zimeshindwa kumudu idadi kubwa ya wagonjwa na kwamba wagonjwa wengi katika Hospitali ya Sabeen katika mji mkuu Sana'a wamelala sakafuni kutokana na uhaba wa vitanda.
Mashambulizi ya kila uchao ya Saudia yamesababisha huduma za afya na matibabu nchini Yemen kukumbwa na mgogoro mkubwa.
Kuendelea mashambulizi hayo ya anga ya Saudia na waitifaki wake katika miundombinu, mahospitali, shule na makazi ya raia na kadhalika mzingiro wa kila upande wa nchi hiyo vamizi dhidi ya Yemen, kumepelekea kuenea kwa kasi maradhi kama vile kipindupindu na magonjwa mengine yanayoteketeza maisha ya wananchi wa Yemen hususan watoto.

0 comments:

Chapisha Maoni