Kutolewa kwa mikanda zaidi ya video za mauaji
yaliyofanywa na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo dhidi ya raia
wa nchi hiyo kumeingiza kashfa hiyo katika awamu mpya.
Mikanda hiyo ya video ya mauaji ya raia iliyoonyeshwa katika
mitanda ya kijamii, imetoa changamoto kubwa kwa serikali ya Kinshasa.
Mikanda hiyo inawaonesha wanajeshi wa serikali ya Congo wakiwaua
kikatili raia wanachama wa kundi la Kamuina Nsapu katika mkoa wa Kasai.
Mmoja kati ya mikanda hiyo ya video ambao ulichukuliwa mwezi Januari
mwaka huu unaonesha picha za kaburi la umati lililogunduliwa eneo al
Kasai.
Awali serikali ya Congo ilidai kuwa filamu hizo ni za kubuni lakini
baadaye mahakama ya nchi hiyo ilianza kushughulikia watu waliohusika na
mauaji ya raia hao.
Hadi sasa watu saba wametiwa nguvuni kwa tuhuma za kutenda jinai
dhidi ya binadamu, kuua na kukata viungo vya miili ya binadamu.
Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, jeshi la serikali ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo liliua wanachama 101 wa kundi la Kamuina Nsapu
katika jimbo la Kasai mwezi uliopita wa Februari.
Wahanga wengi wa mauaji hayo ni watoto na vijana waliopigwa risasi.
Mahakama ya Congo DR imetangaza kwamba inafanya uchunguzi zaidi kuhusu
mauaji hayo.
0 comments:
Chapisha Maoni