Mkuu wa mkoa wa Mbeya Amos Makala amempongeza mkuu wa wilaya ya Mbeya, ndg Nyirembe Munasa na kumshukuru kwa kazi kubwa ya kuirejesha shule ya Sekondari ya Iyunga katika hali yake ya awali na kuiboresha vema baada ya majanga mawili mawili ya moto yaliyotokea mfululizo katika mwezi Machi mwaka huu wakati alipofanya ziara katika shule hiyo leo.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya pia ameishukuru wizara ya TAMISEMI chini ya afisi ya rais kwa kuuvaa uhusika wa kuilea shule ya sekondari Iyunga baada ya kupata matatizo ya moto kwani shule zote za sekondari na msingi nchini Tanzania ziko chini ya wizara ya TAMISEMI.
Akitolea mifano ya methali mbili ambazo ni "ukondefu wa mbwa ni udhaifu wa mwenye mbwa" na "Mafanikio yana marafiki wengi, matatizo mtoto yatima" mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makala amewashukuru watanzania waliotoa michango mbalimbali na kuungana pamoja katija kipindi hiki kigumu cha matatizo ili wanafunzi warejee shuleni aprili mosi. Mkuu wa mkoa pia ameonesha kufurahia kile kinachoonekana sasa katika shule ya Iyunga kwani baada ya majanga ya moto kutokea na kutolewa agizo la kukarabati majengo yaliyoathiriwa na moto, hata yale majengo ambayo hayakuwa katika mpango wa kukarabatiwa nayo pia yanakarabatiwa.
Pamoja na hayo Makala ametoa agizo la kuwekwa hadharani kwa taarifa ya fedha kwa kutanabaisha kila kilichofanyika katika harambee ikiwa ni pamoja na kuthaminisha hesabu zote zilizofanyika na kuwekwa katika makaratasi ya taarifa.
Pamoja na agizo hilo, mkuu wa mkoa wa Mbeya, Amos Makala ametoa agizo la kukarabatiwa mabweni yote ya shule ya Sekondari ya Iyunga na baada ya hapo itafuata kazi ya kukarabatiwa kwa nyumba za waalimu.
Wakati akitoa maagizo hayo Makala amewataka madiwani wote wa halmashauri ya jiji la Mbeya kufanya kazi pamoja naye pasipo kujali itikadi za vyama na kuahidi kuwa atakuwa tayari kushirikiana na kila diwani ili mambo yaende sawa huku akitumia kauli ya 'HAPA KAZI TU'
Shule ya sekondari Iyunga ya hapa jijini Mbeya ilipatwa na majanga mawili ya moto mfululizo kufuatia uchakavu wa miundombinu ya umeme katika majengo ya shule hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni