Ndugu Wanahabari, tukiwa tunaelekea sikukuu ya pasaka, Serikali ya Mkoa wa Dodoma imeona ni vyema ikakutana na wawakilishi wa vyombo vya habari hapa Mkoani Dodoma, ili kupitia vyombo vya habari, tupate fursa ya kuweka wazi kwa wananchi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla masuala ya msingi ambayo yamejiri hapa Mkoani Dodoma.
Awali, usiku wa kuamkia jana kuna tukio tunaloweza kuita la ujambazi lilitokea kama majira ya saa 8 usiku ambapo kundi la watu takribani saba (7) ambao bado hawajafahamika walivamia ofisi za Halotel Mkoani Dodoma kwa lengo la kutaka kufanya uhalifu ambapo waliwavamia askari wawili waliokuwa wakilinda Ofisi hiyo, ambapo pamoja na athari nyingine zilizojitokeza; walipora silaha aina ya SMG na kumjeruhi askari mmoja ambaye alilazwa kwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuruhusiwa jana hiyohiyo.
Hadi hivi sasa Jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kulifanyia kazi suala hilo ambapo hadi tunavyozungumza sasa tayari silaha hiyo iliyoporwa imeshapatikana, uchunguzi zaidi wa suala hilo unaendelea kubaini watu wote waliohusika. Kufuatia suala hilo, Serikali ya Mkoa wa Dodoma, kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana anapenda kutoa tamko lifuatalo:
· Kwanza kabisa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana analaani vikali tukio hilo la uhalifu na kuwa halivumiliki na halikubaliki katika Mkoa wa Dodoma na Mikoa mingine hapa nchini na amewataka wananchi wema kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Dola ili kuwabaini wahusika na kukomesha matukio kama hayo.
· Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana analiagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanafanya uchunguzi na kuwabaini wale wote waliohusika katika tukio hilo la uhalifu,ili kuwatia mbaroni na kuwachukulia hatua kali za kisheria. Aidha amelitaka jeshi la polisi kujipanga vizuri na kuhakikisha kuwa tukio hili ni la mwisho na halijitokezi tukio jingine la aina hii.
· Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna dalili zozote za kuwepo kwa uzembe wa aina yoyote kwa askari hao waliokuwa wanalinda Ofisi hiyo, na endapo itabainika kulikuwa na uzembe basi Jeshi la polisi lichukue hatua kali kwa askari hao waliohusika.
Katika hatua nyingine, Mnamo mwezi Februari kulitokea tukio la mgogoro baina ya jamii za kifugaji za wamaasai na wabarbaig/Mang’ati eneo la mpakani mwa wilaya ya Kondoa kwa upande wa Mkoa wa Dodoma na Wilaya ya Simanjiro kwa Upande wa Mkoa wa Manyara, ambapo Mama mmoja mja mzito jamii ya Kibarbaig akiwa anachunga mifugo aliuwawa na watu inaosemekana ni jamii ya wamasai na kisha mifugo aliyokuwa akichunga (ngombe 25) kuibwa.
Katika kile kinachoonekana kama kulipiza kisasi au kujibu mapigo, wabarbaig nao walivamia kwa wamasai na kuiba ng’ombe 112 ambao baadae walirudishwa kwa wamasai huku Ngombe 25 wakiwashikilia kwa lengo la kutaka kulipwa ng’ombe zao 25 zilizoibiwa wakati zikichungwa na mama wa kibarbaig aliyeuwawa na baada ya wamasai kurudisha ngombe hao 25 na kusaidia aliyehusika na mauaji kupatikana, wabarbaig walirudisha ng’ombe hao 25 wa wamasai waliokuwa wamewashikiria.
Baada ya siku mbili au tatu Wamasai waliibuka na madai kwamba ngombe wao 101wameibiwa na kijana mmoja wa kimasai kukutwa amekufa wakiwashutumu wabarbaig kuhusika na matukio hayo na kudai serikali isimamie ngombe zao hizo zirudishwe na kutaka mtu au watu waliyohusika na wizi na mauaji hayo kupatikana na kukamatwa.
Baada ya uchunguzi ilibainika kuwa kijana huyo wa kimaasai alikutwa amekufa vichakani siyo kwenye boma kama walivyodai wamaasai hapo awali na ilionekana kuwepo kwa dalili kuwa amekufa kabla ya mgogoro huo wa wamaasai na Barbaig kuanza.
Mgogoro huu ulikua na dalili za kutishia amani na usalama wa maeneo yale na jamii zile husika. Kwa muda wote serikali za mikoa miwili ya Dodoma na Manyara kupitia kwa viongozi wao na kamati za ulizi na usalama zilihusika kwa karibu na kuhakikisha athari zaidi hazitokei.
upande wa wafugaji jamii ya kimasai walilalamika serikali kutoshughulikia suala hili ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ng’ombe wao 112 waliokuwa wameibwa na wabarbaig wanarejeshwa, Kufuatia hali hii, Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Manyara na kamati zao za Ulinzi na Usalama za Mikoa yao na Wilaya husika walikubaliana na kutoa maagizo yafuatayo:
· Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana kwanza kabisa amekemea na kulaani vikali matukio hayo ya uhasama na wizi wa mifugo kati ya makundi hayo yenye kuhatarisha usalama na amani ya makundi husika. Vilevile serikali haitavumilia matukio kama hayo ya uvunjifu wa amani badala yake kila mtu/mwananchi anatakiwa kufuata na kutii sheria za nchi bila shuruti.
· Mhe. Rugimbana ameliagiza Jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Polisi Mkoa wa Manyara na viongozi wa kimila kutoka pande zote mbili kwenda nyumba hadi nyumba kutambua wamaasai walioibiwa ng’ombe hao 112 pia na ng’ombe wenyewe walioibiwa, alama zao kisha kufanya msako wa boma hadi boma kubaini ng’ombe hao walioibiwa.
· Wakati wote huo zoezi hilo likiendelea ametaka wananchi kutii sheria za nchi bila shuruti na kuhakikisha wana dumisha usalama na amani wakati wote na endapo baada ya zoezi hilo itabainika shutuma hizi za kuibiwa ng’ombe sio za kweli basi waliotoa shutuma hizi wachukuliwe hatua kali za kisheria.
· Amezipongeza kamati za ulinzi na usalama za Mikoa ya Dodoma na Manyara na viongozi wa Wilaya za Kondoa na Simanjiro kwa kusimamia vizuri utatuzi wa Mgogoro huu na kutaka wazidi kushirikiana na wananchi wao pia ili kulipatia ufumbuzi tatizo hili kwa hali ya amani.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Jordan Rugimbana amepongeza na ameunga Mkono hatua iliyochukuliwa na Naibu waziri Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Suleiman Jafo ya kufanya ziara ya kushtukiza katika ghala la usindikaji ngozi za wanyama lisilo Rasmi eneo la Mailimbili juzi tarehe 24 machi, 2016 ambapo alibaini ghala hilo halifuati taratibu na kanuni za Afya na usafi wa mazingira na kuwa limekuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo na lina hatarisha Afya zao. Mhe. Naibu Waziri Jafo aliamua kulifunga ghala hilo na kuwapa siku tano uongozi wa Manispaa ya Dodoma kuhakikisha ngozi na vitu vyote kwenye ghala hilo vinaondolewa kutokana na kuendeshwa kinyume cha taratibu za Afya.
Katika kuunga mkono hatua alizozifanya Mheshimiwa Naibu Waziri Jafo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana amewaagiza Uongozi wa Manispaa ya Dodoma na Wamiliki na waendeshaji wa ghala hilo wafike Ofisini kwake mara moja kwa lengo la kuzungumzia tatizo hilo na kutafuta namna ya kulimaliza mara moja ili kuhakikisha usalama wa Afya za wananchi waliopo eneo linalozunguka ghala hilo unalindwa, vilevile kuzuia magonjwa yanayoweza kusababishwa na hali hiyo lakini kikubwa ikiwa kutafuta namna bora inayozingatia taratibu za Afya katiika kuanzisha maghala na viwanda vya ngozi.
Mwisho kabisa, Serikali ya Mkoa wa Dodoma inatumia fursa hii kuwataka wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma kusherehekea sikukuu ya Pasaka kwa hali ya Amani, utulivu na Usalama. Na kuwa kila mwananchi ahakikishe anakua balozi mwema kwa kufuata maelekezo haya ya serikali ya Mkoa, pia wamiliki na wasimamizi wa kumbi zote za starehe na burudani wanatakiwa kuzingatia agizo lililotolewa na baraza la sanaa hapa nchini na kuzingatia masharti ya Leseni zao za biashara ikiwa ni pamoja na kutoruhusu madisco ya watoto kwenye kumbi za burudani. vilevile, kumbi za burudani na starehe zifungwe kwa wakati sahihi kwa mujibu wa leseni za biashara za kumbi hizo.
Amewataka maafisa utamaduni wilaya zote kwa kushirikiana na Jeshi la polisi kuhakikisha maagizo haya ya serikali yanatekelezwa ipasavyo.
Mwisho Mkuiu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana anawatakia wananchi wote wa Mkoa wa Dodoma sikukuu njema ya Pasaka.
0 comments:
Chapisha Maoni