Jumanne, Machi 01, 2016

HALMASHAURI YA JIJI LA TANGA KUVUNJWA!?

Serikali imetishia kuivunja Halmashauri ya Jiji la Tanga iwapo haitamaliza mgogoro wake wa kisiasa.
Akizungumza na viongozi serikali na kisiasa jijini Tanga Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema serikali italazimika kuivunja halmashauri hiyo endapo mgogoro huo hautamalizwa haraka, kutokana na ukweli kwamba tangu kuanza kwa uongozi wa awamu ya tano baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana imeshindwa kufanya vikao vyake halali kwa mujibu wa katiba kutokana na mgogoro wa kisisa bina ya Chama Chama cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa, huku wananchi wakishindwa kutatuliwa kero zao kwa wakati hivyo kuzorotesha maendeleo yao.
“Mpaka sasa jiji la Tanga hakuna uongozi uliosimama, sasa hatuwezi kwenda kwa mwendo huu, wananchi wanahitaji maendeleo na kurudia uchaguzi hatuwezi ni gharama kubwa, kilichobaki ni kuivunja halmashauri mpaka hapo muda wa kufanya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya nchi utakapotimia, hivyo kwa maana nyingine kama itavunjwa serikali kuu ndiyo itasimamia shughuli za jiji hili,” alisema Suluhu.
Alisema mkoa huo una mipango mbalimbali ya maendeleo lakini haiwezi kutekelezeka kutokana na mgogoro uliopo na kuwataka viongozi wa mkoa kwa kushirikiana na wazee kukaa chini kutafuta namna ya kuumaliza haraka.
“Jiji ni kioo cha mkoa mzima, sasa kama wazee hawatakaa kitako na viongozi kutafuta suluhu, basi hii mipango yenu yote ya kufufua viwanda itakuwa ni ndoto tu kwa sababu hapa mjini hakupo shwari na tunalitambua hilo,” alisema.
Mgogoro wa umeya Tanga umeibuka baada ya CCM yenye madiwani wachache kushinda nafasi hiyo dhidi ya Ukawa yenye madiwani wengi jambo ambalo linapingwa na umoja huo unaondwa na vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD.

0 comments:

Chapisha Maoni