Jumatano, Februari 17, 2016

MFANYAKAZI WA KIHINDI AFUKUZWA KAZI NCHINI KWA KUWAITA WAFANYAKAZI NYANI

Raia wa India, Dennis Smith ameachishwa kazi katika Hoteli ya Ramada kwa madai ya kuwatukana wafanyakazi wa ngazi za chini akiwaita nyani.
Smith, ambaye ni meneja wa chakula na vinywaji wa hoteli hiyo, aliwatukana na kuwadhalilisha wafanyakazi hao siku ya Sikukuu ya Wapendanao akiwatuhumu kushindwa kuandaa meza vizuri.
Kutokana na udhalilishaji huo, wafanyakazi wa hoteli hiyo jana waligoma wakishinikiza meneja huyo asimamishwe kazi au wao waache kazi.
Wakizungumza jana, baadhi ya wafanyakazi ambao waliomba majina yao yahifadhiwe walisema tabia ya meneja huyo imekuwa sugu na tukio la juzi lilikuwa halivumiliki. Walisema raia huyo wa India amekuwa mwenye majivuno na kutoa lugha chafu dhidi yao.
“Tumechoshwa, anatuitaje sisi nyani, hii tabia ni ya muda mrefu na sasa hatuwezi kuivumilia,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Mwakilishi wa wafanyakazi hao, Mathew Misalaba alisema bosi huyo amekuwa akiwarushia maneno ya kuwadhalilisha kila wanapofanya makosa hata kidogo.
Alisema licha ya uongozi wa hoteli kuahidi kumsimamisha kazi Smith, wamelipeleka suala hilo polisi ili hatua stahiki zichukuliwe.
Meneja Rasilimaliwatu wa hoteli hiyo, Sebastian Nchimbi alisema tayari Smith ameachishwa kazi kutokana na tukio hilo.
“Tulizungumza na wafanyakazi wakatuambia kuwa hawataki Smith awepo kazini na sisi tukafanya uamuzi ili kuwalinda wafanyakazi wetu,” alisema.
Alisema waliamua kumwachisha kazi Smith baada ya kupata malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi hao.
“Si tukio la mara ya kwanza na ndiyo maana tulipoona yamezidi tuliamua kuchukua hatua,” alisema.
Hata hivyo, Nchimbi alimsifu Smith akisema ni mtendaji mzuri na alikuwa na tija kwa hoteli hiyo ya kitalii lakini hakuwa na kauli nzuri kwa wafanyakazi Waafrika.
“Kiutendaji ni mzuri mno… yaani kwetu sisi tunapoteza mtu hasa, tatizo ni mdomo tu,” alisema.

0 comments:

Chapisha Maoni