Jumatatu, Februari 08, 2016

DRC MABINGWA WA SOKA AFRIKA

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetwaa ubingwa wa Michuano ya Mabingwa wa Soka katika Mataifa ya Afrika maarufu kama CHAN baada ya kuitia skulini Mali kwa kuisasambua mabao 3-0. 
Katika kitimutimu hicho cha fainali kilichofanyika katika uwanja wa taifa wa Amavubi mjini Kigali, Rwanda, vijana wa DRC walionyesha mchezo mzuri katika takriban kipindi chote na hatimaye kutwaa Kombe la CHAN kwa mara ya pili, tangu michuano hiyo ya kibara ianzishwe mwaka 2009. 
Nyota wa mchuano huo alikuwa kiungo Mechak Elia ambaye alicheka na nyavu za Mali mara mbili, huku mshambuliaji Jonathan Bolingi akifunga bao moja.
Ushindi huo wa pili kwa Kongo DR chini ya mkufunzi Florent Ibenge kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya Afrika umeingia katika madaftari ya kumbukumbu. Huku hayo yakijiri, Kodivaa imemaliza katika nafasi ya tatu katika michuano hiyo baada ya kuichabanga Guinea Mabao 2-1 katika kindumbwendumbwe cha kumtafuta mshindi wa tatu. 
Rais wa Rwanda Paul Kagame alikuwa katika uwanja wa Amavubi kuwatuza vijana wa DRC, ingawa alitamani taji hilo lingetwaliwa na wenyeji wa mashindano hayo vijana wa Amahoro. Mbali na taji hilo, DRC wametia kibindoni dola laki 7 na elfu 50 za Marekani, huku Mali na Ivory Coast zikiondoka na dola laki 4 na dola laki 2 na nusu za Marekani kwa usanjari huo. 
Kenya itakuwa mwenyeji wa michuano ijayo ya CHAN mwaka 2018.

0 comments:

Chapisha Maoni