Mshambuliaji hodari wa Real Madrid Cristiano Ronaldo amezua mjadala mkali baada ya kutoa matamshi yaliyoonekana kulaumu wachezaji wenzake baada ya kushindwa nyumbani 1-0 na Atletico Madrid hapo juzi (Jumamosi).
"Tungekuwa wa kwanza iwapo wachezaji wote wangeweza kucheza kama mimi," Ronaldo aliambia waandishi wa habari. "Sitaki kukosea mtu heshima, lakini ni vigumu kushinda wakati wachezaji bora hawako uwanjani," alisema akionekana kufedheheshwa. "Ningependa kucheza na Pepe, Karim, Gareth Bale...Marcelo... Sijasema kuwa Jese, Lucas na (Mateo) Kovacic ni wachezaji duni." alisema Cristiano.
Real Madrid hawakuwa na mchezaji Gareth Bale ambaye ana jeraha. Karim Benzema aliondoka wakati wa mapumziko kufuatia jeraha huku Jese Rodriguez na Lucas Vazquez wakiingia uwanjani kipindi cha pili.
Real Madrid sasa wamesalia katika nafasi ya tatu kwenye jedwali ya ligi ya Hispania, pointi tisa nyuma ya Barcelona FC ambao wanaogoza ligi hiyo na pointi 63. Matamshi ya Ronaldo yamezua hisia mbali mbali kwenye mitandao ya jamii na kugonga vichwa vya habari za spoti duniani.
0 comments:
Chapisha Maoni