Jumanne, Januari 12, 2016

WENYE MISIMAMO MIKALI WAANDAMANA DHIDI YA WAISLAMU UJERUMANI

Mamia ya watu wenye chuki za kidini wanaowapiga vita Waislamu na Uislamu nchini Ujerumani PEGIDA wamefanya maandamano na kuzusha hali ya mchafukoge katika mji wa Leipzid nchini humo.
Waandamanaji hao waliokuwa wameficha nyuso zao wamechoma moto magari, kuvunja maduka na kuripua mafataki katika majengo ya makazi na kibiashara katika wilaya ya Connewitz mjini Leipzid. Katika maandamano hayo ya jana Jumatatu mbali na watu hao wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu kutumia jukwaa hilo kuonyesha chuki zao dhidi ya Uislamu na Waislamu, walikuwa wanaadhimisha kumbukumbu ya kuanzishwa kundi lenye misimamo mikali la mrengo wa kulia la PEGIDA la nchini Ujerumani. Haya yanajiri siku chache baada ya Baraza la Waislamu la nchini Ujerumaini kutahadharisha kuhusu kuongezeka vitendo vinavyotokana na chuki za kidini dhidi ya Waislamu nchini humo. Baraza hilo limetangaza kuwa, chuki dhidi ya Waislamu na dhidi ya wageni zimeongezeka nchini Ujerumani baada ya watu wasiojulikana kuwapora na kuwadhalilisha wanawake katika mji wa Cologne katika mkesha wa mwaka mpya wa 2016. Itakumbukwa kuwa, Oktoba mwaka jana kundi la PEGIDA lilitoa wito kuwa Waislamu barani Ulaya wapelekwe kwenye kambi za mateso makali kama zile zilizokuwepo wakati wa utawala wa Kinazi nchini Ujerumani.

0 comments:

Chapisha Maoni