Jumatatu, Januari 11, 2016

WAKATI SHEREHE ZA MAPINDUZI ZIKIFANYIKA LEO, CUF WASEMA HAWANA NIA YA KUVURUGA AMANI ZANZIBAR

Wakati maadhimisho ya miaka 52 ya MAPINDUZI YA ZANZIBAR yakifanyika leo visiwani humo, Chama cha Wananchi cha nchini Tanzania (CUF) kimelaumu njama zinazofanywa na baadhi ya watu za kutaka kusababisha machafuko visiwani Zanzibar kwa kushikilia kurudiwa uchaguzi visiwani humo.
Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa, chama hicho hakitakubali kurudiwa uchaguzi huo.
Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mgombea wa urais wa tiketi ya chama cha Wananchi CUF katika uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015, amesema kuwa, hakuna mashiko yoyote ya kisheria yanayoweza kuhalalisha hatua ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha ya kutangaza kufutwa uchaguzi huo na kusema kuwa, uchaguzi wa Oktoba 25 ni halali.
Baadhi ya viongozi wa chama cha CCM wamejitokeza hadharani na kutanga kuunga mkono kurudiwa uchaguzi visiwani Zanzibar na kuwataka wafuasi wao visiwani humo kujiandaa kwa jambo hilo. Hata hivyo chama cha CUF kimelaani vikali matamshi hayo na kusema yanalenga kukwamisha mazungumzo yanayoendelea hivi sasa Zanzibar ya kuutafutia ufumbuzi mkwamo wa kisiasa uliovikumba visiwa hivyo.

0 comments:

Chapisha Maoni