Alhamisi, Januari 07, 2016

MAHAKAMA IMEZUIA KUBOMOLEWA KWA JUMBA LA MAMA KWAKATARE, SABABU?!

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi imezuia nyumba anayoishi Mchungaji wa Kanisa  la  Assemblies of God Mikocheni, Dk. Getrude Lwakatare kubomolewa.
Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa juzi na Jaji John Mgeta, baada ya Wakili wa Lwakatare, Emmanuel Muga kuwasilisha maombi ya kupinga ubomoaji huo chini ya hati ya dharura.
Jaji Mgeta alizuia ubomoaji wa jengo hilo ama kuchukua hatua yoyote kuhusu jengo hilo lililopo Kawe Beach.
Muga aliwasilisha maombi akimwakilisha mdai ambaye ni mtoto wa Mchungaji Lwakatare, Robert Brighton dhidi ya wadaiwa NEMC, Manispaa ya Kinondoni na wadau wengine wote.
“Mheshimiwa jaji, nawasilisha maombi ya zuio la kubomoa nyumba ya mteja wangu chini ya kifungu namba 95 cha Sheria ya Mwenendo wa Madai na kifungu namba 2(3) cha JALA vinavyotoa mamlaka kwa mahakama kutoa nafuu stahili pale kunapokuwa na ukiukwaji wa kuvunja haki ya wazi,” alidai.
Akitoa uamuzi huo alisema tayari pande husika zilikuwa na kesi namba 70 ya mwaka 2012 na ikamalizika kwa kutoa hukumu na kukazia hukumu iliyompa haki ya ushindi mdai.
“Mahakama ilimpa haki mdai, lakini chakushangaza mdaiwa anakiuka matakwa ya hukumu na kutaka kubomoa nyumba, kwa hali isiyokuwa ya kawaida mdai anahitaji ulinzi wa mahakama hii ya haki,”alisema Jaji Mgeta.
Alisema nyumba hiyo ipo katika kiwanja namba 2019 na 2020 ambapo hati yake ilitolewa mwaka 1979.
Inadaiwa mwaka 2011 NEMC ilitoa notisi ya kuvunja nyumba hiyo baada ya kushinikizwa na wakazi wa eneo hilo wakidai ujenzi wake unaziba Mto Ndumbwi na uko jirani na mikoko.
Wakili Muga aliwasilisha maombi ya kuzuia nyumba  ya mteja wake kubomolewa  baada ya Wizara  ya  Maliasili  na  Utalii kupitia  wakala  wa  misitu  Tanzania (TFS ), kuweka alama  ya X wakidai imo katika hifadhi  ya  bahari.

0 comments:

Chapisha Maoni