BENKI Kuu (BoT) imeitoza faini Benki ya Stanbic Sh bilioni tatu baada ya kubaini benki hiyo imefanya miamala ya kutia shaka inayohusu malipo kwa kampuni ya Kitanzania ya EGMA ya Dola za Marekani mil.6 zilizoingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo na kutolewa ndani ya muda mfupi.
Stanbic iliwezesha Serikali ya Tanzania kuuza hati fungani za dola milioni 600 (Sh trilioni 1.3) kwa benki ya Standard Chartered ya Uingereza. Mauzo hayo yalifanyika mwaka 2012 kwa Serikali kwa masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4; lakini Stanbic tawi la Tanzania iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya Serikali ya Tanzania kutakiwa kulipa riba ya asilimia 2.4.
Adhabu iliyotangazwa jana na Serikali kwa benki hiyo, inatokana na Stanbic kuilipa EGMA Dola za Marekani milioni 6 ambazo ziliingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo ya kitanzania na kutolewa kwa muda mfupi kwa njia ya fedha taslimu, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za kibenki.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philipo Mpango alisema BoT katika uchunguzi wake, imebaini malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume na taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa Benki ya Stanbic.
Dk Mpango alisema BoT imechukua hatua ya kutoza faini benki hiyo kama onyo iweze kuwa makini katika kuhakikisha shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki za kuzingatia sheria.
“Hatua hii ni onyo kwa benki na taasisi zingine za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hiyo ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema Dk Mpango.
Waziri alifafanua kuwa sheria inaitaka Benki ya Stanbic kutoa utetezi katika siku 20 ambazo zitaisha Januari 30 mwaka huu.
“Endapo BoT haitaridhika na utetezi wake, Benki ya Stanbic italazimika kulipa faini hiyo,” alisema.
Alisema hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Uchunguzi wa BoT
Akielezea hatua za uchunguzi huo, Dk Mpango alisema taarifa ya uchunguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic kwa mujibu wa taratibu na BoT iliagiza bodi ya wakurugenzi ya benki kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana.
Alisema benki hiyo pia iliagizwa kutoa taarifa kwa kitengo kinachochunguza makosa ya fedha (FIU) kilichoko Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu miamala hiyo yenye mashaka katika akaunti ya EGMA kama sheria ya kuzuia utakatishaji wa fedha haramu inavyoelekeza.
“Benki ya Stanbic ilitekeleza maagizo na kutoa taarifa FIU kuhusu miamala hiyo iliyotiliwa shaka,” alisema Dk Mpango.
Dk Mpango alisema ripoti hiyo ya BoT pia iliombwa kutumiwa na Shirika la Upelelezi la Makosa Makubwa (SFO) katika kesi dhidi ya Benki ya Standard ambayo waliruhusu itumiwe kwa kuzingatia chanzo cha ripoti hiyo.
“Hatimaye Standard ilikubali makosa na ilitozwa faini ya jumla ya dola za Marekani milioni 32.20 na kiasi cha dola za Marekani milioni saba zinalipwa kwa Serikali ya Tanzania,” alisema Dk Mpango na kufafanua kuwa dola milioni 6 zilikuwa ni fidia na dola milioni moja ni riba.
Takukuru yawahoji
Akijibu maswali ya waandishi wa habari ambao walitaka kufahamu wahusika wengine wamechukuliwa hatua gani, Dk Mpango alisema bado Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inaendelea na uchunguzi katika makosa yanayohusu rushwa.
“Hili ambalo limefanyika leo ni kuhusu uchuguzi wa BoT kuhusu masuala ya miamala ya kifedha, sasa kuna vyombo vingine vya dola vinaendelea kuwahoji wahusika na wakikamilisha kazi yao watatangaza hatua za kuchukua,” alisema Dk Mpango.
0 comments:
Chapisha Maoni