Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, nchini Tanzania
Jaji Joseph Warioba amewataka Watanzania kutokurupuka kuipitisha Katiba
Inayopendekezwa kwa kuwa imeyaacha kando maoni yao mengi.
Jaji Joseph
Warioba amewataka Watanzania waisome kwa makini katiba hiyo kabla ya
kuikubali au kuikataa. Jaji Warioba amesema, Katiba hiyo haina maoni
yote ya wananchi kama Bunge Maalumu lilivyojinadi, bali yamewekwa
machache ambayo hata hivyo yamo hata katika Katiba ya sasa.
Warioba
amesema, wananchi wengi walipendekeza kiwepo kipengele cha maadili ya
viongozi ili kuwadhibiti dhidi ya vitendo viovu wanavyovifanya kwa sasa
kama ufisadi, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, lakini wajumbe wa
Bunge walikirekebisha hadi kikapoteza maana.
Vile vile Jaji Warioba
amebainisha kwamba, wananchi walipendekeza muundo wa muungano wa
serikali tatu ili kuondoa kero na matatizo yaliyopo, kupatiwa madaraka
ya kuwawajibisha wabunge wao pamoja na rais kupunguziwa madaraka, mambo
ambayo yameondolewa na Bunge hilo Maalumu.
Tayari mrengo wa upinzani
nchini Tanzania chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA umetangaza
kwamba, utatembea nchi nzima kuwahamasisha Watanzania waikatae Katiba
hiyo ambayo wanasema imepuuza na kuweka kapuni maoni ya wananchi
waliowengi.
0 comments:
Chapisha Maoni