Dilma Rousseff amejipatia ushindi kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa
rais nchini Brazil, baada ya kumshinda kwa taabu hasimu wake wa kisiasa
Aecio Neves aliyegombea kwa tiketi ya Brazilian Social Democracy Party
(PSDB) kwa asilimia 51.6 ya kura zilizopigwa.
Tume ya Taifa ya
Uchaguzi ya Brazil imetangaza kuwa, Neves amejipatia asilimia 48.4 ya
kura zote zilizohesabiwa. Jumla ya watu milioni 143 waliotimiza masharti
ya kupiga kura walishiriki kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa rais
nchini Brazil.
Rousseff kutoka chama cha Wafanyakazi, amefanikiwa kujipatia ushindi
kutokana na uungaji mkono mkubwa wa tabaka la watu masikini, ambao
wamezikubali sera za chama hicho katika kushughulikia masuala ya
kijamii.
Sera za serikali ya Rais Rousseff zimeweza kuwatoa watu
milioni 40 kutoka kwenye lindi la umasikini, na kuwaweka katika maisha
ya wastani. Dilma Rousseff mwenye umri wa miaka 66 alichaguliwa kwa mara
ya kwanza kuiongoza Brazil mwaka 2010, na katika duru ya kwanza ya
uchaguzi iliyofanyika 5 Oktoba mwaka huu, alijipatia asilimia 41.5 ya
kura na mpinzani wake Neves kujipatia asilimia 33.5 na hivyo uchaguzi
huo kulazimika kuingia duru ya pili.
0 comments:
Chapisha Maoni