Ijumaa, Oktoba 17, 2014

MATUKIO MAKUBWA 6 KUTOKA MBEYA LEO

KATIKA TUKIO LA KWANZA:

Mtembea kwa miguu mmoja aliyetambulika kwa jina la Tunsume Mbope (35) mkazi wa Kyela amefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na pikipiki yenye namba za usajili T.496 CRL aina ya Kinglion iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika jina wala makazi yake.
Ajali hiyo imetokea jana majira ya saa moja na nusu jioni huko Mafula Sop, kata ya Kyela, tarafa ya Unyakyusa, wilaya Kyela, mkoa wa Mbeya. Chanzo cha ajali kinachunguzwa. Dereva alikimbia mara baada ya ajali na juhudi za kumtafuta zinaendelea. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya kyela.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi anatoa wito kwa madereva kuwa makini wanapotumia vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Aidha, anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo mtuhumiwa [dereva] azitoe katika mamlaka husika ili akamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

KATIKA TUKIO LA PILI:

Mtoto mwenye umri wa miaka 05 aliyetambulika kwa jina la Isack Jacob mkazi wa kijiji cha Ilundo alifariki dunia baada ya kuangukiwa na mti uliokuwa unakatwa na wanafunzi wa shule ya sekondari Kiwira iliyopo wilaya ya Rungwe.
Tukio hilo limetokea mnamo jana saa 11:00 asubuhi katika maeneo ya shule ya sekondari Kiwira, kata ya Kiwira, tarafa ya Ukukwe, wilaya ya Rungwe, mkoa wa Mbeya.
Inadaiwa kuwa, marehemu alikuwa akiokota kuni na watoto wenzake vichakani na ndipo aliangukiwa na mti huo na kupelekea kifo chake.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi anatoa wito kwa wazazi/walezi kuweka uangalizi wa kutosha kwa watoto wadogo ili kuepuka madhara yanayoweza kuepukika. Aidha, anatoa wito kwa jamii kutowaruhusu watoto wadogo kwenda maeneo ya vichakani/porini bila kuwa na watu wazima kwani ni hatari.

TAARIFA ZA MISAKO:

Watu wanne waliofahamika kwa majina ya 1. Zakayo Nova (27) 2. Hamadi Ngeka (27) wote wakazi wa Tunduma 3. Yona Siwale (23) mkazi wa kijiji cha Chiwanda na 4. Ezekia Sikaponda (33) mkazi wa Chitete wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Mbeya wakiwa na ng’ombe wanne wanaodhaniwa kuwa mali ya wizi.
Watuhumiwa hao walikamatwa mnamo tarehe 16.10.2014 majira ya saa 05:00 alfajiri huko katika machinjio ya Tunduma, mtaa wa Sogea, kata na tarafa ya Tunduma, wilaya ya Momba, mkoa wa Mbeya.
Inadaiwa kuwa, ng’ombe huo ni mali ya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Lusangia Jihumbi, mkazi wa Chitete. Aidha, thamani ya halisi ya ng’ombe hao ni tshs.2,400,000/=. Ng’ombe hao wamehifadhiwa kituo cha polisi tunduma wakisubiri taratibu nyingine za kisheria.

KATIKA MSAKO WA PILI

Mtu mmoja raia wa nchini Malawi anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Mbeya kwa kosa la kuingia nchini kinyume cha sheria. Mhamiaji huyo amefahamika kwa jina la Alfred Rungu (40) alikamatwa mnamo tarehe 16.10.2014 majira ya saa 08:50 asubuhi huko stendi ya mabasi Tukuyu mjini, kata ya Kawetele, tarafa ya Tukuyu mjini, wilaya ya Rungwe, mkoa wa Mbeya. Taratibu za kumkabidhi idara ya uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea.

KATIKA MSAKO WA TATU,

Mtu mmoja mkazi wa Rift Valley wilaya ya Chunya aitwaye Lucy Edward (25) anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Mbeya akiwa na pombe haramu ya moshi ujazo wa lita 20.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 16.10.2014 majira ya saa 17:30 jioni huko katika kitongoji cha Rift Valley, kijiji cha Malangamilo, kata ya Mkola, tarafa ya Kiwanja, wilaya ya Chunya, mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa ni mtengenezaji na muuzaji wa pombe hiyo.

KATIKA MSAKO WA NNE

Mtu mmoja mkazi wa Chianga nchini Zambia aliyefahamika kwa jina la George Sikamanga (18) anashikiliwa na jeshi la polisi mkoa wa Mbeya akiwa na kete 85 na gramu 10 za bhangi.
Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 16.10.2014 majira ya saa 19:45 jioni huko eneo la Custom, kata na tarafa ya Tunduma, wilaya ya Momba, mkoa wa Mbeya katika msako ulioendeshwa na jeshi la polisi katika maeneo hayo. Mtuhumiwa ni muuzaji wa bhangi hiyo na taratibu za kumfikisha mahakamani zinaendelea.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa jamii kuacha kutumia pombe ya moshi/dawa za kulevya kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya ya mtumiaji.

0 comments:

Chapisha Maoni