WATU wawili, Dilu Tungu (80) na mwanawe
Bunya Mihangwa (45) wameuawa kikatili kwa kuchinjwa na watu
wasiofahamika baada ya kuvamia nyumba hiyo katika kijiji cha Ihugi kata
ya Lyamidati wilaya ya Shinyanga kwa kile kilichoelezwa kuwa ni imani za
kishirikina.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa
wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema kuwa tukio hilo lilitokea Oktoba
14 mwaka huu saa mbili usiku katika kijiji cha Ihugi, kata ya Lyamidati
tarafa ya Nindo wilaya ya Shinyanga.
Akielezea zaidi kuhusu tukio hilo
alisema siku hiyo, Dilu na mtoto wake Mihangwa, wote wakazi wa Ihugi
wakiwa nyumbani kwao wakijiandaa kwa chakula cha usiku na wanafamilia
wenzao walivamiwa na watu watatu wasiofahamika wakiwa na mapanga.
Baada ya kuwavamia walianza kuwakata kwa panga sehemu mbalimbali za miili yao kisha kuwachinja shingo hadi wakapoteza maisha
alisema Kamanda Kamugisha.
Alisema kuwa chanzo cha tukio hilo ni
imani za kishirikina kutokana na kile kilichodaiwa kuwa mwanamume
aitwaye Bwanya Mlyashimba (40), mkazi wa Ihugi alikuwa akiwatuhumu Dilu
na mwanawe Mihangwa kwamba walimroga yeye mwenyewe na kusababisha akose
nguvu za kiume.
Alisema mbali na Mlyashimba kuwatuhumu
kumroga, pia alikuwa anawatuhumu kumroga mama yake aitwaye Hollo
Mahangwa aliyefariki dunia mwaka 2013.
Akasema Jeshi la Polisi linamshikilia
mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi huku likiendelea kuwasaka wahusika
wengine wa mauaji hayo.
0 comments:
Chapisha Maoni