Jumatano, Oktoba 29, 2014

MADAKTARI 5000 WANAHITAJIKA KUPAMBANA NA EBOLA

Mkuu wa Benki ya Dunia (WB) amesema kuwa nchi za magharibi mwa Afrika zinahitaji madaktari na wauguzi elfu tano kwa ajili ya kukabiliana na homa ya virusi hatari vya Ebola.
Jim Yong ambaye alikuwa akizungumza mjini Addis Ababa nchini Ethiopia ameashiria hofu iliyosababishwa na ugonjwa hatari wa Ebola na akaeleza wasiwasi wake juu ya njia za kupatikana wahudumu hao wa afya katika nchi za Magharibi mwa Afrika.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye pia amehutubia kikao hicho, amesema kasi ya kuenea virusi vya Ebola ni kubwa zaidi kuliko ile ya juhudi za jamii ya kimataifa za kukabiliana na janga hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma amesema kuwa nchi wanachama wa umoja huo zimeahidi kutuma zaidi wa wataalamu 2000 wa afya na matibabu katika nchi za Magharibi mwa Afrika. Hata hivyo Zuma hakuashiria lini wahudumu hao watatumwa katika nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa Ebola ambao kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) umeshaua karibu watu elfu tano.

0 comments:

Chapisha Maoni